" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAADHIMISHA MIAKA 49 YA CCM KWA KUPANDA MITI

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAADHIMISHA MIAKA 49 YA CCM KWA KUPANDA MITI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini leo Januari 26, 2026 imeadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi Ujamaa iliyopo Seseko, Kata ya Mwamalili, Manispaa ya Shinyanga.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya wiki ya maadhimisho ya miaka 49 ya CCM, ikiwa na lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Mgeni rasmi katika zoezi hilo ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, Bi. Regina Ndulu, ambaye ametumia fursa hiyo kuhamasisha wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kupanda miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili iweze kuleta tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko, amesema jumuiya hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuimarisha afya za wananchi.

Mzee Fue ameeleza kuwa Jumuiya ya Wazazi CCM itaendelea kuhamasisha wanachama wake kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira, ikiwemo upandaji na uhifadhi wa miti, kama njia ya kulinda vyanzo vya maji, kupunguza ukame na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa maisha ya binadamu.

Aidha, Katibu Regina Ndutu pamoja na Mwenyekiti Mzee Fue wametumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa hatua zake nzuri katika kusambaza nishati safi ya kupikia, ikiwemo matumizi ya mitungi ya gesi, huku wakiwahamasisha wananchi kuendelea kutumia nishati safi ili kuepukana na ukataji wa miti unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Viongozi hao wameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ni suluhisho muhimu katika kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kupunguza madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wao, baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Wazazi CCM wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji, wamesema wataendelea kushirikiana kwa karibu na serikali pamoja na viongozi wa chama ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, hususan katika maeneo ya mazingira, afya na maendeleo ya jamii.

Kwa ujumla, shughuli hiyo imeonesha mshikamano wa wanachama wa CCM katika kuenzi misingi ya chama chao kwa vitendo, huku ikitafsiri maadhimisho ya miaka 49 ya CCM kama fursa ya kutoa mchango chanya kwa jamii na kuendelea kujenga taifa lenye mazingira salama na maendeleo endelevu.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, Bi. Regina Ndulu, akizungumza na wanachama wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya CCM yaliyofanyika Wilaya ya Shinyanga Mjini.Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko, akizungumza kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kuunga mkono juhudi za serikali.

Katibu wa Mbunge Jimbo la Shinyanga mjini Samwel Jackson akitoa salamu za mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Paschal Patrobas Katambi.




Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Naibu Katalambula akizungumza kwa niaba ya katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya hiyo.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post