" AFISA ELIMU SEKONDARI MANISPAA YA SHINYANGA AIPONGEZA SHY TALENT FILMS KWA KUANDAA DRAMA YA ELIMU

AFISA ELIMU SEKONDARI MANISPAA YA SHINYANGA AIPONGEZA SHY TALENT FILMS KWA KUANDAA DRAMA YA ELIMU

Picha ya pamoja.

Kikundi cha sanaa cha SHY Talent Films leo Januari 21, 2026 kimeendelea na mazoezi na uonyeshaji wa drama yenye ujumbe wa elimu, hatua inayoendelea kuonesha dhamira ya kutumia sanaa kama nyenzo ya kuelimisha na kuhamasisha jamii katika Manispaa ya Shinyanga.

Mgeni rasmi katika mazoezi hayo ni Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Makoye Richard, ambaye ameipongeza Taasisi ya Misalaba Media kwa kuanzisha kikundi cha SHY Talent Films, akieleza kuwa ni wazo lenye maono makubwa linalotoa fursa kwa vijana kuibua na kuendeleza vipaji vyao sambamba na kutoa elimu kwa jamii.

Akizungumza na wanakikundi hicho, Mwalimu Makoye Richard amewatia moyo vijana kutokukata tamaa, akisisitiza kuwa mbele kuna fursa nyingi zitakazowanufaisha endapo wataendelea kuwa na nidhamu, uvumilivu na malengo yaliyo wazi na kwamba Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa vikundi hicho kwa kuwa kinatumia sanaa kuelimisha jamii na kujenga maadili mema, hususan katika masuala ya elimu.

Ameongeza kuwa sanaa ni njia muhimu ya kufikisha ujumbe kwa jamii kwa urahisi, hasa kwa vijana na wanafunzi, hivyo jitihada zinazofanywa na SHY Talent Films zina mchango mkubwa katika kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya elimu.

Katika mazoezi hayo pia Mkuu wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, Mwalimu Marko Msangwa, naye amepongeza drama ya elimu iliyooneshwa na kikundi hicho, akisema imegusa kwa kina changamoto zinazowakabili wanafunzi wengi katika safari zao za kielimu na maisha ya kila siku.

Pia amesema ujumbe uliobebwa kwenye drama hiyo unaakisi hali halisi ya jamii na unahitaji kuendelea kufikishwa kwa umma.

Kabla ya viongozi hao kutoa maoni yao, kikundi cha SHY Talent Films kilionyesha drama yenye ujumbe unaogusa sekta ya elimu, hasa changamoto zinazojitokeza katika jamii ikiwemo upotoshaji wa taarifa, ushawishi mbaya na maamuzi yasiyo sahihi yanayoweza kuwaathiri wanafunzi wa shule za sekondari.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa taasisi, Mkurugenzi wa Misalaba Media, Mapuli Misalaba, ameeleza dhana na dhamira ya kuanzisha kikundi hicho, akisema lengo kuu ni kuibua vipaji vya vijana na kutumia sanaa kama jukwaa la kutoa elimu, kuhamasisha mabadiliko chanya na kujenga jamii yenye uelewa.

Kwa upande wake Meneja wa Misalaba Media, Daniel Sibu, ameeleza malengo ya drama iliyooneshwa, akibainisha kuwa inalenga kuibua mjadala kuhusu changamoto za elimu zilizopo katika jamii na kwamba changamoto hizo zipo na hata Mkuu wa Shule alikiri kuwa ujumbe uliotolewa kwenye drama unaendana na hali halisi inayojitokeza katika mazingira ya shule.

Mwenyekiti wa SHY Talent Films, Daniel Elimboto, kwa niaba ya wanakikundi, amewashukuru wageni hao kwa kushiriki mazoezi hayo na kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwaunga mkono vijana, akisema ushirikiano huo utaisaidia SHY Talent Films kufikisha ujumbe kwa jamii kwa ufanisi zaidi.

Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Makoye Richard, akizungumza na wanakikundi cha SHY TALENT FILMS baada ya kushuhudia drama ya elimu leo Januari 21, 2025.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga Mwalimu Marko Msangwa , akitoa maoni baada ya kuangalia drama ya elimu iliyoandaliwa na SHY TALENT FILMS.

Mkurugenzi wa Misalaba Media, Mapuli Misalaba, akieleza dhamira ya kuanzishwa kwa kikundi cha SHY TALENT FILMS katika kutumia sanaa kuelimisha jamii.

Meneja wa Misalaba Media na Katibu wa SHY TALENT FILMS DanieL Sibu, akifafanua malengo ya drama ya elimu na changamoto zinazogusa sekta ya elimu.









  

 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post