" POLISI SHINYANGA WAMSHIKILIA MWANAMKE KWA TUHUMA ZA KUMCHOMA MOTO MUMEWE

POLISI SHINYANGA WAMSHIKILIA MWANAMKE KWA TUHUMA ZA KUMCHOMA MOTO MUMEWE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina Mwajuma Shaban anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa tuhuma za kumwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto mume wake kufuatia mgogoro wa wivu wa mapenzi uliotokea katika Mtaa wa Mageuzi, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza na Misalaba Media, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), amesema tukio hilo lilitokea Machi 5, 2026 majira ya saa sita usiku.

Amesema majeruhi ametambulika kwa jina la David Mollis mwenye umri wa Miaka 34, dereva wa bodaboda na mkazi wa Mtaa wa Mageuzi ambapo inadaiwa kuwa wakati akiwa amekaa sebuleni nyumbani kwake, alijeruhiwa baada ya kumwagiwa mafuta ya petroli na kuwashiwa moto na mke wake na kusababisha kupata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kifuani na mkononi.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mwanamke anayehusishwa na tukio hilo ni Mwajuma Shaban Mwenye umri wa Miaka 24 ambaye pia ni mkazi wa mtaa huo na alikuwa akiishi pamoja na David kama mke na mume.

Amesema chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi, ambapo mwanamke huyo alidai kuwa alimkopesha mume wake kiasi cha shilingi 80,000 na baadaye kuhisi kuwa fedha hizo zimetolewa kwa mwanamke mwingine.

Kamanda Magomi amesema kuwa majeruhi anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga huku uchunguzi ukiendelea ili mtuhumiwa aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kamanda huyo amelaani kitendo hicho na kutoa wito kwa wanandoa na jamii kwa ujumla kuepuka vitendo vya ukatili na badala yake kutatua migogoro kwa kufuata taratibu za kisheria.

Amesema Jeshi la Polisi lina madawati maalum yanayoshughulikia ukatili wa kijinsia na kusisitiza kuwa ukatili unaweza kuwakumba wanawake, watoto pamoja na wanaume.

Wakati huo huo, Misalaba Media imefika katika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya majirani wakiwemo wapangaji wenzake Cesilia John, Lucy Shija pamoja na jirani Bi. Rosemary Mboje, ambao wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo majira ya saa sita usiku.

Majirani hao wamesema hawakuwa na taarifa ya mgogoro wowote kati ya wanandoa hao kabla ya tukio hilo kutokea, ambapo wameeleza kuwa baada ya tukio hilo walifanikiwa kumzuia mwanamke huyo ili asikimbie hadi jeshi la Polisi lilipofika.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wasafirishaji Bodaboda Mitumbani Kata ya Ngokolo, Jacobo Msimbang’ombe, amesema amesikitishwa na tukio hilo lililompata mwanachama wao na kuwataka madereva wa bodaboda kushirikishana changamoto wanazokutana nazo ili kupata suluhisho kabla ya madhara makubwa kutokea.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mageuzi, Vitalis Mugisha, amesema alipigiwa simu na mmiliki wa nyumba aliyopanga David na kufika katika eneo la tukio kabla ya kutoa taarifa kwa viongozi mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi ili hatua zaidi zichukuliwe.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia njia za kisheria kutatua migogoro.

    

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post