
Wananchi wamehimizwa kuendelea kuthamini, kuenzi na kuhifadhi utamaduni wa Kitanzania unaojenga maadili mema, umoja wa kitaifa na maendeleo ya kijamii, huku wakitakiwa kuachana na mila potofu zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Wito huo umetolewa na viongozi wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii ya SMAUJATA wakati wa ziara ya Kanda ya Ziwa iliyofanyika mkoani Mara.
Ziara hiyo ilihusisha mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ikiwa na lengo la kutathmini hali ya ukatili katika Mkoa wa Mara na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda amani, kuhifadhi utamaduni na kupinga vitendo vya ukatili.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii Taifa wa SMAUJATA, Shujaa Hashim Omary, kwa kushirikiana na Mkuu wa Idara hiyo Taifa, Shujaa Daniel Kapaya, alisema utamaduni ni urithi muhimu unaobeba historia, mila, desturi na utambulisho wa Taifa, hivyo unapaswa kuhifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo huku ukiondoa mila zote zinazokiuka haki za binadamu.
Viongozi hao walieleza kuwa utamaduni pia ni nguzo muhimu ya maendeleo kupitia sekta ya utalii, sanaa, michezo ya asili, mavazi ya jadi, vyakula vya asili na kazi za mikono, ambazo huchangia kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa SMAUJATA ulitembelea makundi mbalimbali ya kijamii na kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji, ubakaji, ndoa za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia. Pia ulihimiza wananchi kuendelea kulinda amani na mshikamano kwa maendeleo ya Taifa.
Ujumbe huo ulipata nafasi ya kutembelea Kituo cha Nyumba Salama cha HOPE Women Girls kilichopo Wilaya ya Butiama, ambapo ulizungumza na wahudumu pamoja na kutoa elimu kuhusu ulinzi wa wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili. Aidha, ulitembelea Makumbusho ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyopo Mwitongo, Butiama, kwa lengo la kujifunza historia na kuhamasisha wananchi kuenzi misingi ya uzalendo, umoja na uongozi wa Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Alfred Mtambi, aliushukuru uongozi wa SMAUJATA kwa kuchagua Mkoa wa Mara kuwa sehemu ya ziara hiyo na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na idara hiyo katika kuelimisha jamii. Alisema SMAUJATA imekuwa chombo muhimu kinachowafikia wananchi moja kwa moja kwa kutoa elimu kuhusu kupinga ukatili na kuhimiza amani.
Kanali Mtambi alisisitiza kuwa elimu hiyo inapaswa kuendelea kutolewa kwa nguvu zaidi kwa kuwa inasaidia kubadili mitazamo ya wananchi na kupunguza vitendo vya ukatili vinavyotokana na mila potofu. Aliongeza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya sekta zote za uchumi, ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji na shughuli nyingine za uzalishaji.
Viongozi wa SMAUJATA walitoa shukrani kwa Wakuu wa Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuwapa katika utekelezaji wa kampeni za elimu kwa jamii kuhusu kupinga ukatili, kuhifadhi utamaduni na kuimarisha amani.
SMAUJATA imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii, kuhamasisha uhifadhi wa utamaduni, kuondoa mila potofu na kujenga Taifa lenye amani, mshikamano na maendeleo endelevu.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254












Post a Comment