" RUTAZIKA AWAHIMIZA WALIMU KUZINGATIA MTAALA MPYA, MANISPAA YA SHINYANGA YAFANYA MAFUNZO ELEKEZI

RUTAZIKA AWAHIMIZA WALIMU KUZINGATIA MTAALA MPYA, MANISPAA YA SHINYANGA YAFANYA MAFUNZO ELEKEZI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Mkoa wa Shinyanga, Dedan Rutazika, amewahimiza walimu wa shule za sekondari kuuelewa kwa kina Mtaala Mpya Ulioboreshwa wa Elimu ya Sekondari na kuutekeleza kwa ufanisi ili kufanikisha malengo ya elimu na kuinua ufaulu wa wanafunzi.

Rutazika ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa walimu yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga leo Januari 22,2026, ambayo yamelenga kuwajengea uelewa na kuongeza uwezo wa walimu katika utekelezaji wa mtaala mpya.

Katika hotuba yake, ameipongeza Idara ya Elimu Sekondari ya Manispaa ya Shinyanga kwa kuendelea kuzingatia mabadiliko ya mitaala ya elimu na kuandaa mafunzo yanayolenga kuwajengea walimu uelewa wa kina juu ya mabadiliko hayo.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya mitaala yanahitaji walimu kuwa na uelewa wa falsafa ya mtaala, mbinu za kisasa za ufundishaji na namna bora ya kumjenga mwanafunzi kimaarifa na kivitendo huku akisisitiza kuwa mafunzo elekezi ni nyenzo muhimu inayowawezesha walimu kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujiandaa ipasavyo kwa utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Taaluma Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Richard Makoye, ameeleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea walimu uelewa wa namna bora ya kuandaa na kutumia zana za kufundishia na kujifunzia kwa kuzingatia mtaala mpya ulioboreshwa.

Amesema kupitia mafunzo hayo, walimu wanajengewa uwezo wa kuandaa mipango ya ufundishaji, kutumia mbinu shirikishi za ujifunzaji na kutathmini umahiri wa wanafunzi kwa kuzingatia matakwa ya mtaala.

Mwalimu Makoye ameongeza kuwa uboreshaji wa ufundishaji wa masomo ya sayansi, sayansi ya jamii na elimu ya biashara ni hatua muhimu katika kuongeza ufaulu na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua changamoto na kujitegemea kielimu na kijamii.

Nao baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Idara ya Elimu Sekondari ya Manispaa ya Shinyanga kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yamewasaidia kuongeza maarifa na uelewa wao kuhusu mtaala ulioboreshwa, hususan katika masomo ya kidato cha kwanza na pili.

Wamesema uelewa walioupata utachangia kuboresha ufundishaji darasani, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao za kielimu.

Mafunzo hayo yamewakutanisha takribani walimu wawakilishi 170 kati ya walimu 496 kutoka shule 22 za sekondari zilizopo ndani ya Manispaa ya Shinyanga na kwamba yamewahusisha walimu wa masomo ya sayansi, sayansi ya jamii pamoja na elimu ya biashara, masomo ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kujenga uelewa, stadi na umahiri wa wanafunzi kulingana na mabadiliko ya mtaala mpya.

Kupitia mafunzo hayo, Manispaa ya Shinyanga inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuinua kiwango cha elimu ya sekondari kwa kuwekeza katika rasilimali watu, hususan walimu, kama nyenzo muhimu ya kufanikisha mabadiliko ya elimu.

Hatua hiyo inaendana na kaulimbiu ya Manispaa hiyo isemayo “Shinyanga Municipal, Let Us Push Together,” inayohamasisha ushirikiano wa wadau wote katika maendeleo ya elimu na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga na Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Mkoa wa Shinyanga, Dedan Rutazika, akizungumza na walimu wa shule za sekondari wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya utekelezaji wa Mtaala Mpya Ulioboreshwa yaliyoandaliwa na Manispaa ya Shinyanga.

Afisa Elimu Taaluma Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Richrad Makoye, akieleza malengo ya mafunzo elekezi kwa walimu wa shule za sekondari kuhusu mbinu bora za kufundishia na kutumia zana za kujifunzia chini ya Mtaala Mpya Ulioboreshwa.

Afisa Elimu Taaluma Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Richrad Makoye, akieleza malengo ya mafunzo elekezi kwa walimu wa shule za sekondari kuhusu mbinu bora za kufundishia na kutumia zana za kujifunzia chini ya Mtaala Mpya Ulioboreshwa.


Walimu wa shule za sekondari wakishiriki kwa bidii mafunzo elekezi yaliyofanyika Manispaa ya Shinyanga, yakilenga kuongeza uelewa na uwezo wao katika utekelezaji wa Mtaala Mpya Ulioboreshwa wa Elimu ya Sekondari.





  

Post a Comment

Previous Post Next Post