Na Mapuli Kitina Misalaba
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya
Shinyanga Mjini imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika
wilaya hiyo, ikisisitiza umuhimu wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati ili
wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotarajiwa.
Ziara hiyo imefanyika leo Machi 10, 2026 ikiongozwa na
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe, ambapo kamati
hiyo imetembelea miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa standi mpya ya mabasi ya mkoa,
ujenzi wa soko kuu la Shinyanga pamoja na mradi wa uboreshaji wa barabara ya
kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Katika ziara hiyo, kamati ya siasa ilianza kwa
kutembelea Shule ya Msingi Bugayambelele ambako Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa
chumba kimoja cha darasa ili kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa
shuleni hapo.
Baada ya hapo kamati hiyo ilitembelea mradi wa ujenzi
wa standi mpya ya mabasi ya Mkoa wa Shinyanga unaoendelea katika Kata ya
Kizumbi na kwamba wakati wa ukaguzi wa mradi huo, kamati hiyo ilibaini kuwepo
kwa changamoto mbalimbali ikiwemo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi
wanaofanya vibarua katika mradi huo.
Baadhi ya wafanyakazi hao walisema wanalipwa ujira
mdogo ambao hauendani na viwango vinavyotakiwa kisheria, huku wakidai pia
kucheleweshewa malipo yao kwa takribani mwezi mmoja ambapo walisema licha ya
kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato, bado malipo yao yanachelewa na
kiasi wanachopewa hakiridhishi.
Akizungumza baada ya kusikiliza malalamiko hayo,
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe amesema kamati
hiyo imezipokea changamoto hizo na kuahidi kuzifuatilia ili kuhakikisha haki za
wafanyakazi zinazingatiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo imetembelea mradi
wa ujenzi wa Soko Kuu la Mkoa wa Shinyanga ambapo wafanyabiashara wameendelea
kueleza kilio chao cha kutaka mradi huo ukamilike haraka ili waweze kurejea
kufanya biashara zao.
Mwenyekiti wa soko hilo amesema wakati wafanyabiashara
wanahamishwa kutoka eneo la soko walielezwa kuwa ujenzi ungechukua miezi sita
pekee kwani mafundi wangefanya kazi mchana na usiku, lakini hadi sasa ni
takribani miaka minne imepita bila mradi kukamilika.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mjini, Mhe. Salum
Kitumbo amewaomba wafanyabiashara kuwa na subira huku akiwahakikishia kuwa
hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kwa kushirikiana na wataalam ili
kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unakamilika kwa ubora na kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe.
Makombe amesema amepokea changamoto hizo na kuahidi kuwa chama kitaendelea
kufuatilia ili kuona mradi huo unakamilika na wananchi wanaanza kunufaika nao.
Katika ziara hiyo, kamati ya siasa pia imekagua mradi
wa uboreshaji wa barabara ya kutoka Nguzonane kuelekea Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Shinyanga inayojengwa kwa kiwango cha lami. Hata hivyo kamati hiyo
haikuridhishwa na mwenendo wa mradi huo.
Wananchi pamoja na madiwani wa Kata ya Ndani Mhe.
Zamda Shaban na Diwani wa Kata ya Masekelo Mhe. Piter Koliba wamesema viongozi
mbalimbali wa serikali wamewahi kutembelea mradi huo na kutoa maelekezo,
akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Shinyanga Mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga
Wakili Julius Mtatiro, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita pamoja na
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi.
Hata hivyo wamesema pamoja na maelekezo hayo,
mkandarasi hajachukua hatua madhubuti na mradi huo umesimama kwa zaidi ya wiki
moja bila kazi kuendelea kufanyika.
Kwa mujibu wa viongozi hao, mradi huo una mkataba wa
miezi 15 lakini hadi sasa baada ya miezi saba kupita umefikia takribani
asilimia 14 tu ya utekelezaji hali inayoonyesha kusuasua kwa ujenzi huo huku
wakisisitiza hatua zaidi zichukuliwe ikiwemo kumwondoa mkandarasi endapo
ataendelea kuchelewesha mradi huo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti Makombe amesema
kamati hiyo imepokea malalamiko hayo na itaendelea kufuatilia ili kubaini
changamoto zilizopo na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa.
Aidha, kamati hiyo imetembelea Shule ya Sekondari ya
Wasichana Shinyanga Girls ambapo imekagua ujenzi wa bweni pamoja na miundombinu
mingine ya shule hiyo na kwamba viongozi wa kamati hiyo wametumia fursa hiyo
kuishauri serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka uzio kuzunguka
shule hiyo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa wanafunzi.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo imetembelea Soko la
Mitumbani lililopo Kata ya Ngokolona ambapo imesikiliza changamoto
zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo.
Wafanyabiashara wameeleza kuwa baadhi ya miundombinu
ya soko hilo siyo rafiki, hususan kipindi cha mvua ambapo maeneo mengi hujaa
maji na kufanya mazingira ya biashara kuwa magumu.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ni endelevu na inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ilani ya chama hicho kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokusudiwa na serikali.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua maendeleo ya ujenzi wa standi mpya ya mabasi ya Mkoa wa Shinyanga inayojengwa katika Kata ya Kizumbi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe, akizungumza.
Diwani wa Kata ya Mjini, Mhe. Salum Kitumbo akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa standi mpya ya mabasi.
Samwel Jackson katibu wa mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini akizungumza.
Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga alikataa kuzungumzia malalamiko ya vibarua wake.
Mmoja wa wananchi wanaofanya vibarua katika mradi wa ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga akieleza malalamiko yake.
Mmoja wa wananchi wanaofanya vibarua katika mradi wa ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga akieleza malalamiko yake.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe.
Anord Makombe, akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa soko kuu la Mkoa wa Shinyanga.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua mradi wa uboreshaji wa barabara ya kutoka Nguzonane kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua mradi wa uboreshaji wa barabara ya kutoka Nguzonane kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe.
Anord Makombe, akitoa maelekezo baada ya kutembelea uboreshaji wa barabara ya Mwawaza.
Mkuu wa shule ya sekondari Shinyanga Girls Mwalimu Nurah Wilfred akisoma taarifa fupi ya shule hiyo.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua ujenzi wa bweni na miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga Girls.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua ujenzi wa bweni na miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga Girls.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikikagua ujenzi wa bweni na miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga Girls.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikitembelea Soko la Mitumbani lililopo Kata ya Ngokolo.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ikisikiliza changamoto za wafanyabiashara katika Soko la Mitumbani lililopo Kata ya Ngokolo.🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254














Post a Comment