" JAMBO GROUP YATAJWA KUWA KIELELEZO CHA UWEKEZAJI WA WAZAWA NCHINI

JAMBO GROUP YATAJWA KUWA KIELELEZO CHA UWEKEZAJI WA WAZAWA NCHINI

Na Mapuli Kitina Misalaba

SERIKALI imeeleza kuwa uwekezaji wa viwanda, hususan vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo na mifugo, ni nguzo muhimu ya kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, huku ikitoa pongezi kwa Jambo Group of Companies kwa mchango wake mkubwa katika ajira, ulipaji kodi na maendeleo ya sekta ya maziwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 9, 2026 mkoani Shinyanga wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, waliotembelea kiwanda cha Jambo Group kinachojihusisha na uchakataji wa maziwa na bidhaa za matumizi ya kila siku (FMCG).

Akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo, Mkurugenzi  wa Jambo Group Khamis Salum ameeleza kuwa Jambo ni kiwanda cha Kitanzania kilichoanzishwa kwa dhamira ya kuwa mfano kwa wawekezaji wengine wazawa, akisisitiza kuwa Watanzania wana uwezo mkubwa wa kujenga viwanda vikubwa na endelevu.

Katika upande wa ajira, ameeleza kuwa Jambo Group inaajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 wa kudumu, huku ajira za muda na zisizo za moja kwa moja zikifikia zaidi ya watu 10,000, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana na wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group Mhe. Salum Khamis Mbuzi ameeleza kuwa mradi wa maziwa unaotekelezwa na Jambo Group una thamani ya dola za Marekani milioni 45, huku thamani ya jumla ya kiwanda hicho kwa sasa ikifikia takribani shilingi trilioni 1.2. Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, miradi hiyo inalenga kujenga uchumi wa wananchi na kuchangia moja kwa moja kwenye mapato ya Serikali.

Ameongeza kuwa Jambo Group imeamua kuwa mzalendo kwa kulipa kodi kwa uwazi na uaminifu, ambapo kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kampuni hiyo kwa sasa inachangia takribani shilingi bilioni 12 kwa mwezi na kwamba kampuni imeendelea kuwa miongoni mwa walipa kodi wakubwa hususan katika Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, ameeleza kuwa mwelekeo wa Serikali kwa sasa umejikita zaidi kwenye uwekezaji, kwa lengo la kuwapatia wakulima na wafugaji masoko ya uhakika ya mazao yao.

Amesema kuwa Tanzania ina wakulima na wafugaji wengi, lakini changamoto kubwa imekuwa ni kukosekana kwa maeneo ya kupeleka mazao ili yaweze kuongeza thamani na kuleta faida halisi kwa wananchi ambapo kwa msingi huo, anasema Serikali inahitaji wawekezaji kama Jambo Group wanaoamua kuwekeza kwenye viwanda vinavyowagusa wananchi moja kwa moja.

Naibu Waziri huyo ameipongeza kampuni ya Jambo Group kwa mchango wake katika ajira, akieleza kuwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 wa kudumu na takribani 10,000 wa muda ni mchango mkubwa kwa Taifa huku akiongeza kuwa ili uchumi wa nchi uendelee kukua, ni lazima Serikali na sekta binafsi ziwekeze zaidi kwenye viwanda, hususan vya watu binafsi na mashirika ya umma.

Ametoa wito kwa wawekezaji wengine kuiga mfano wa Jambo Group, akisisitiza kuwa ni mwekezaji wa Kitanzania aliyeamua kujitoa kusaidia jamii na kwamba Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono jitihada za uwekezaji wa kampuni hiyo ili kuhakikisha kiwanda kinaendelea kukua na kuongeza ajira kwa manufaa ya wakulima na wafugaji, hususan wa Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amefikisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita iko tayari kutekeleza yote yaliyoahidiwa kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi huku akiwaomba wananchi na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na kumuombea Rais ili aendelee kuliongoza Taifa kwa hekima na mafanikio.

Waziri huyo amesema kuwa ameridhishwa na hatua zote za maendeleo alizoziona katika kiwanda cha Jambo Group, akisisitiza kuwa milango ya Serikali iko wazi kutoa huduma na kuwezesha wawekezaji katika sekta zote. Anafafanua kuwa changamoto zitakazoshindikana kutatuliwa katika ngazi ya wizara zitapelekwa kwa Waziri Mkuu, na endapo zitahitaji maamuzi ya juu zaidi, zitafikishwa kwa Makamu wa Rais na hatimaye kwa Rais.

Anaeleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuweka mazingira salama na rafiki kwa wafugaji, wavuvi, wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji, ili Tanzania iweze kujenga uchumi imara, shindani na unaojitegemea.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameeleza kuwa uwepo wa Jambo Group Mkoani Shinyanga ni fahari kubwa kwa Mkoa na ni ushahidi wa vitendo kuwa Shinyanga ni eneo salama na rafiki kwa uwekezaji.

Ameeleza kuwa miradi mikubwa kama hiyo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuongeza ajira, kipato cha kaya na mzunguko wa fedha katika maeneo ya vijijini na mijini.

Mhe. Mhita amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wawekezaji wote wanaokuja Shinyanga, kwa kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanabaki kuwa tulivu, salama na yenye ushirikiano, ili Mkoa uendelee kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group Mhe. Salum Khamis Mbuzi  akieleza mchango wa kiwanda hicho katika ajira, ulipaji kodi na maendeleo ya sekta ya maziwa leo wakati wa ziara ya viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Group Mhe. Salum Khamis Mbuzi  akieleza mchango wa kiwanda hicho katika ajira, ulipaji kodi na maendeleo ya sekta ya maziwa leo wakati wa ziara ya viongozi wa Serikali mkoani Shinyanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akizungumza wakati wa ziara ya kikazi kiwandani hapo, akieleza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa viwanda katika kuwasaidia wakulima na wafugaji kupata masoko ya uhakika.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akizungumza kuhusu umuhimu wa uwekezaji wa Jambo Group katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Shinyanga.

Mkurugenzi  wa Jambo Group Khamis Salum, akisoma taarifa fupi ya kampuni hiyo leo Ijumaa Januari 9, 2026 wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji katika kiwanda hicho.



 


Post a Comment

Previous Post Next Post