" JUKWAA LA VIJANA KUZINDULIWA: SERIKALI YAFUNGUA ENZI MPYA YA USHIRIKI, UBUNIFU NA MUSTAKABALI WA VIJANA

JUKWAA LA VIJANA KUZINDULIWA: SERIKALI YAFUNGUA ENZI MPYA YA USHIRIKI, UBUNIFU NA MUSTAKABALI WA VIJANA

Katika kuelekea kilele cha dira ya maendeleo ya taifa, serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana, inatarajia kuzindua rasmi Jukwaa la Vijana (Youth Platform), tukio ambalo linatajwa kuwa mwarobaini wa changamoto na mashaka mbalimbali yanayowakabili vijana nchini. 

Uzinduzi huo unaotarajiwa kufanyika Januari 10, 2026, katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam na utaongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka.

Uzinduzi wa jukwaa hili unakuja wakati muafaka, ukiwa na lengo kuu la kutoa nafasi mahsusi kwa vijana kusemea changamoto zao na kuunganisha nguvu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi. Kwa muda mrefu, vijana wamekuwa na kiu ya kuwa na sehemu rasmi itakayowasikiliza na kuthamini sauti zao, huku jukwaa hili likitarajiwa kutoa fursa za ushiriki wa moja kwa moja katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Umuhimu wa jukwaa hili unajidhihirisha katika hitaji la kuondoa mashaka miongoni mwa vijana kuhusu mustakabali wa maisha yao, hususan katika masuala ya ajira, ujasiriamali na ubunifu. Badala ya kuonekana kama kundi la kulalamika, jukwaa hili linawaandaa vijana kuwa injini ya maendeleo na si injini ya uharibifu. Kupitia jukwaa hili, vijana wataweza kukuza mawazo bunifu yatakayochangia kukuza uchumi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Uwepo wa Wizara mahsusi ya Vijana na kuanzishwa kwa jukwaa hili ni ushahidi tosha kuwa serikali inatambua kuwa vijana ndio nguvu kazi kuu ya taifa. Ni hatua inayolenga kuhakikisha kuwa nguvu hiyo kubwa haipotei, bali inaelekezwa katika uzalishaji na ujenzi wa nchi. Jukwaa hili linatoa fursa kwa vijana kujifunza, kushirikiana na kupeana miongozo ya jinsi ya kufikia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.

Mgeni rasmi katika tukio hilo, Dkt. Joel Nanauka, anatarajiwa kutoa dira ya jinsi wizara itakavyotumia jukwaa hilo kuratibu masuala ya vijana kwa ufanisi zaidi. Hii ni fursa ya kipekee ambapo vijana wanakumbushwa kuwa mabadiliko ya nchi yamo mikononi mwao, na kwamba ushiriki wao katika majukwaa kama haya ndio utakaowezesha sauti zao kufika kwenye meza za maamuzi.

Wadau wa maendeleo wameeleza kuwa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana ni hatua ya kihistoria itakayoziba pengo la mawasiliano kati ya serikali na vijana. Wananchi na vijana wote nchini wanahimizwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo ili kuwa sehemu ya mabadiliko chanya na kuhakikisha kuwa mustakabali wa Tanzania unajengwa kwa misingi ya kazi, utu, na ubunifu wa hali ya juu.

 



Post a Comment

Previous Post Next Post