" SHULE YA MSINGI MASUNULA YAONGOZA KWA MIAKA 9 MFULULIZO, MBUNGE WA ITWANGI AZZA HILLAL HAMAD ATOA ZAWADI, SERIKALI YATOA UHAKIKA WA KUTATUA CHANGAMOTO

SHULE YA MSINGI MASUNULA YAONGOZA KWA MIAKA 9 MFULULIZO, MBUNGE WA ITWANGI AZZA HILLAL HAMAD ATOA ZAWADI, SERIKALI YATOA UHAKIKA WA KUTATUA CHANGAMOTO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, ameendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu katika jimbo hilo kwa kusisitiza upatikanaji wa elimu bora, mazingira salama ya ujifunzaji na ufaulu wenye tija kwa watoto wa Itwangi, akisema maendeleo ya jimbo hilo hayawezi kufikiwa bila kuwekeza kwa dhati katika elimu ya msingi.

Mhe. Azza amesema msimamo wake ni kuhakikisha shule zote za msingi ndani ya jimbo la Itwangi zinafanya vizuri kitaaluma, huku walimu wakifanya kazi katika mazingira yanayowawezesha, ambapo ameendelea kuwasisitiza wazazi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika malezi na ufuatiliaji wa elimu ya watoto wao.

Amesema jitihada hizo tayari zinaanza kuonekana katika baadhi ya shule, ikiwemo Shule ya Msingi Masunula iliyopo Kata ya Usule, ambayo kwa miaka tisa mfululizo imekuwa ikiongoza katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini.

Katika taarifa ya shule ya Masunula, mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wazazi, viongozi wa kijiji, kamati ya shule na vyombo vya ulinzi vya jadi vya Sungusungu, licha ya changamoto zilizopo ikiwemo uchakavu wa madarasa, uhaba wa walimu na tatizo la upatikanaji wa maji shuleni.

Katika kuendeleza ajenda hiyo ya elimu, Mbunge Azza amesisitiza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa sikivu kwa changamoto za elimu, na kwamba kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi na wizara husika, changamoto hizo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

“Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, na ninaamini kupitia Waziri wa Elimu kama alivyoahidi, changamoto za Shule ya Msingi Masunula zitakwenda kutatuliwa. Mimi kama mwakilishi wenu nitaendelea kuwasemea ili kuhakikisha Jimbo la Itwangi linakwenda kung’ara na watoto wetu wanapata ufaulu mzuri katika shule zetu zote,” amesema Mhe. Azza.

Katika hatua ya utekelezaji wa dhamira hiyo, Mbunge Azza ameandaa hafla maalum ya kuipongeza Shule ya Msingi Masunula kwa mafanikio yake ya kitaaluma, ikiwa ni sehemu ya kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi, pamoja na kutoa funzo kwa shule nyingine ndani ya jimbo hilo.

Katika hafla hiyo, Mbunge huyo amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa bidii na kujituma, akisema licha ya changamoto walizonazo, wameamua kusimama na kuhakikisha watoto wa Masunula wanapata matokeo bora huku akipongeza mchango wa wazazi, kamati ya shule, viongozi wa kijiji na Sungusungu katika kulinda na kuimarisha mazingira ya shule.

Aidha, Mbunge Azza ametoa zawadi kwa walimu wa shule hiyo pamoja na kuwapongeza wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2026, akieleza kuwa motisha ni nyenzo muhimu katika kuendeleza mafanikio ya elimu.

Wakati huo huo, serikali kupitia Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoeimetoa hakikisho la kushughulikia changamoto zinazokabili Shule ya Msingi Masunula baada ya Mbunge Azza kuwasilisha rasmi hoja na mahitaji ya shule hiyo kwa niaba ya wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Masunula kwa njia ya simu, Waziri huyo amesema tayari amepokea taarifa zote kuhusu shule hiyo, akimhakikishia Mbunge na wananchi kuwa serikali ipo pamoja nao na kwamba changamoto zote zilizobainishwa zitafanyiwa kazi.

Prof. Riziki Shemdoe amesema licha ya kutofika katika hafla hiyo kutokana na majukumu ya kikazi, ataweka Shule ya Msingi Masunula kwenye ratiba ya ziara zake atakapofanya ziara mkoani Shinyanga, na kusisitiza kuwa utekelezaji wa ahadi hizo utaonekana kwa vitendo.

Katika hafla hiyo, Mbunge Azza pia amewashukuru wananchi wa Jimbo la Itwangi kwa kumwamini na kumchagua katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, akiahidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali za jimbo hilo kwa kushirikiana na serikali.

Kwa upande wa uongozi wa shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masunula Daudi Shineneko amesema mafanikio ya shule hiyo yametokana na nidhamu ya wanafunzi, ushirikiano mzuri kati ya walimu na wazazi pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa masomo ambapo amesema licha ya changamoto zilizopo, walimu wameendelea kufanya kazi kwa kujituma, huku wakisisitiza kuwa lengo lao ni kuona shule hiyo inaendelea kushika nafasi za juu zaidi kitaaluma.

Akizungumzia mchango wa halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dkt. Kalekwa Kasanga amesema mafanikio ya Shule ya Msingi Masunula ni fahari kwa halmashauri hiyo, akibainisha kuwa elimu bora ni kipaumbele cha halmashauri na kwamba ofisi yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanya tathmini ya changamoto zilizopo na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa ameipongeza shule hiyo kwa matokeo bora, akisema mafanikio hayo yanadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa serikali, walimu na wananchi huku akiahidi kuwa baraza la madiwani litaendelea kuisimamia sekta ya elimu na kuunga mkono jitihada zote zinazolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini Edward Ngelela amepongeza uongozi wa Mbunge wa Jimbo la Itwangi kwa kuipa kipaumbele elimu, akisema jitihada hizo zinaakisi utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo amesisitiza kuwa chama kitaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na endelevu.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Masunula wamemshukuru Mbunge wao Mhe. Azza kwa kuendelea kusimamia maendeleo ya shule hiyo na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana na walimu, serikali ya kijiji na viongozi wengine ili kudumisha nidhamu ya wanafunzi na kuhakikisha mafanikio ya shule yanaendelea kuimarika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na maafisa elimu, watendaji wa kata, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, walimu kutoka shule mbalimbali za msingi katika halmashauri hiyo, wazazi, wananchi, baadhi ya wahitimu, madiwani kutoka kata mbalimbali za Jimbo la Itwangi pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi akiwemo katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga vijijini Erinestina Richard na Katibu wa UWT Wilaya ya Shinyanga vijijini Bi. Magreth Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza katika hafla hiyo.Mbunge wa Jimbo la Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad akizungumza kwa njia ya Simu na Waziri wa TAMISEM Prof. Riziki Shemdoe.Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dkt.Kalekwa Kasanga akizungumza.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Masunula Daudi Shineneko akisoma taarifa ya shule.







  

Post a Comment

Previous Post Next Post