" WAZIRI MKENDA AZINDUA UGAWAJI WA MAGARI KWA WATHIBITI  UBORA NA VIFAA  SAIDIZI KWA  WAKUFUNZI NA WALIMU WENYE ULEMAVU

WAZIRI MKENDA AZINDUA UGAWAJI WA MAGARI KWA WATHIBITI  UBORA NA VIFAA  SAIDIZI KWA  WAKUFUNZI NA WALIMU WENYE ULEMAVU

Na.Alex Sonna-DODOMA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Prof. Adolf F. Mkenda, amezindua ugawaji wa magari manne kwa ajili ya wathibiti ubora wa shule pamoja na vifaa vya kielimu vya kidigiti saidizi vyenye thamani ya Sh bilioni 5.3 kwa walimu, wakufunzi na walimu tarajali wenye mahitaji maalum.

Akizungumza kwenye hafla hiyo  iliyofanyika leo Januari 5, 2026, Mtumba,jijini Dodoma,Prof. Mkenda amesema kuwa ugawaji huu ni utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, iliyozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na yenye lengo la kuhakikisha elimu jumuishi na yenye ubora kwa wote bila ubaguzi.

“Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Mheshimiwa Rais kutekeleza mageuzi makubwa ya elimu nchini. Leo tunashuhudia kwa vitendo jitihada za Serikali za kutoa vifaa vinavyosaidia walimu na wakufunzi wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika shughuli za ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Waziri Mkenda.

Prof.Mkenda ametaja vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta mpakato 688, mashine za braille 19, vinasa sauti vya kidijitali 377, kompyuta kibao 196, embosser 6, vikuza sauti 7, vifaa vya tathmini ya uoni na usikivu, programu 5 za Duxbury braille translator, Perkins brailler 130, karatasi za braille 3,000, vifaa vya braille 91 vya “universal kits”, maboksi ya karatasi 2,290, vifaa vya kusikia 121, magongo 11, chupa za mafuta maalumu 3,556, kofia 86, viti mwendo vya kielektroniki 2, viti mwendo vya kawaida 3 na fimbo nyeupe 7.

Amesema kuwa wanaonufaika na vifaa hivyo ni walimu, wakufunzi na wanafunzi wenye ulemavu wakiwemo: watu 342 wenye ulemavu wa viungo, 310 wenye uoni hafifu, 155 wenye uziwi, 90 wenye ualbino, 158 wenye usikivu hafifu, walimu tarajali 63 na wakufunzi 20 wenye ulemavu.

Prof. Mkenda amesema vifaa hivi vitasaidia kuondoa vikwazo vya kimazingira na kiufikikaji, kuboresha mbinu za ufundishaji, kuongeza uhuru na kujitegemea kwa walimu, wakufunzi na wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja na kuinua ufaulu wa kitaaluma.

Aidha, Waziri amesisitiza kuwa magari na vifaa hivyo vinapaswa kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na wanufaika wanawajibika kutunza, kuripoti hali na matumizi yake ipasavyo.

Hata hivyo  ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha elimu jumuishi, huku ikizingatia makubaliano ya kimataifa kama Tamko la Salamanca (1994), Mpango wa Dakar (2000), Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (2006) na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) namba 4 yanayosisitiza upatikanaji wa elimu bora kwa wote.

Serikali pia imetoa mafunzo kwa wadau 21,898 wa sekta ya elimu, ikiwemo viongozi wa vyuo vikuu, walimu, wakufunzi, wahadhiri, wathibiti ubora wa shule, maafisa elimu maalum na wanafunzi wenye mahitaji maalum. Mafunzo haya yallenga kuboresha mbinu za ufundishaji jumuishi na matumizi ya teknolojia saidizi katika vyuo na shule za taifa.

Prof. Mkenda amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha elimu maalumu na jumuishi kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa walimu wa elimu maalumu, kuongeza miundombinu rafiki, na kuhakikisha upatikanaji wa vitabu na vifaa vinavyowezesha walimu na wanafunzi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujifunzaji.

“Hii ni hatua ya kihistoria inayothibitisha dhamira ya Serikali kuhakikisha hakuna mwanafunzi wala mwalimu anayebaki nyuma kutokana na changamoto za ulemavu au mazingira,” amesema Waziri Mkenda.

Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia, Dk.Omar Hussein, amesema kuwa katika hafla hiyo magari manne yametolewa kwa ajili ya wadhibiti ubora yaliyogharimu kiasi cha Sh.milioni 900.4.

"Tulikuwa na upungufu wa magari 23 baada ya haya manne ambayo  yametolewa leo inafanya upungufu kuwa magari 19 lakini lengo ni kufika maeneo yote nchini kuwa na magari kwa ajili ya wadhibiti ubora,"amesema Dk.Hussein

Hata hivyo, amesema  kwa upande wa vifaa saidizi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia kwa watu wenye mahitaji maalum serikali imegharamia kiasi cha Sh. bilioni 5.3 ambavyo vitasambazwa kwenye halmashauri zote nchini

   

Post a Comment

Previous Post Next Post