" MAUAJI YA SOPHIA ZAKALIA: POLISI KAGERA WAHAKIKISHA MTUHUMIWA ATAPATIKANA

MAUAJI YA SOPHIA ZAKALIA: POLISI KAGERA WAHAKIKISHA MTUHUMIWA ATAPATIKANA

 

‎Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.

‎Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30, Sophia Zakalia, mfanyabiashara wa ndizi na mkazi wa Kata ya Katoma, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

‎Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, SACP Blasius Chatanda, amesema mwili wa marehemu ulipatikana Januari 15, 2026, ukiwa umetupwa shambani katika eneo la kata hiyo.

‎Kamanda Chatanda ameeleza kuwa mwili wa marehemu ulikutwa umefungwa kwa kamba, huku sehemu zake za siri zikionekana kuingiziwa kitu butu, hali inayoashiria tukio hilo kufanyika kwa ukatili mkubwa.

‎Aidha, amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mauaji hayo yanahusishwa na tukio la kulipiza kisasi, na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa wa tukio hilo.

‎Kamanda Chatanda ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuacha kujichukulia sheria mkononi, badala yake washirikiane na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha vitendo vya mauaji na uhalifu kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post