Na Ngonise Kahise, Misalaba Media-Dar Es Salaam
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) amesaini mikataba mitano ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani 24,996,672 (zaidi ya Shilingi bilioni 63), hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa utalii nchini.
Mikataba hiyo imesainiwa Januari 16, 2026 kati ya TAWA na Kampuni ya GBP Trading Ltd katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Uwekezaji huo umejikita katika maeneo ya uhifadhi yanayosimamiwa na TAWA, yakiwemo Hifadhi ya Mpanga–Kipengere, Hifadhi ya Kijereshi na Hifadhi ya Wami–Mbiki, ambapo utahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya utalii ikiwemo malazi na huduma kwa watalii.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania.
Amesema kampeni hizo zimeongeza imani ya wawekezaji na kuchangia ongezeko la idadi ya watalii kutoka milioni 1.5 hadi milioni 2.2, huku watalii wa ndani wakifikia milioni 3.2, na kwa takwimu za Novemba 2025, idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia tisa.
“Sekta ya utalii iko imara na mazingira ya uwekezaji ni rafiki. Serikali ya Awamu ya Sita imeweka sera na mifumo inayowavutia wawekezaji, na wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wake ili taifa linufaike,” amesema Dkt. Abbasi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajab Semfuko amesema mikataba hiyo itaongeza vitanda 190 vya malazi ya watalii na kuingiza mapato ya takribani Shilingi bilioni 9.2 kwa mwaka.
Amesema TAWA imeandaa mkakati wa miaka mitano wa kuongeza mapato (2025–2030) unaolenga kuiwezesha mamlaka hiyo kujitegemea kifedha ifikapo mwaka 2027/28 kwa kuzalisha Shilingi bilioni 189 kwa mwaka.
Naye Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Bw. Mlage Yussuf Kabange amesema mbali na mapato ya Serikali, uwekezaji huo utanufaisha moja kwa moja jamii zinazozunguka hifadhi kupitia ajira, miradi ya maendeleo ya jamii na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Amesema TAWA itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kuzitaka sekta binafsi na wadau wengine kuchangamkia fursa zilizopo ili kuimarisha uhifadhi endelevu na kukuza uchumi wa Taifa.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment