Taasisi ya habari ya Misalaba Media imeanzisha kikundi cha sanaa kinachoitwa SHY TALENT FILMS, chenye lengo la kuibua vipaji,
kutengeneza filamu na tamthilia zenye ujumbe wa kuelimisha jamii, pamoja na
kutoa fursa kwa vipaji mbalimbali ikiwemo waigizaji wa maigizo, filamu na
wachekeshaji (stand up comedy).
Hatua hiyo inalenga
kutumia sanaa kama nyenzo ya kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii, huku
ikitoa jukwaa la wazi kwa vijana wenye vipaji kuonyesha uwezo wao na kujijenga
kitaaluma.
Leo Januari 10, 2026, Misalaba Media imefanikiwa kufanya
kikao cha pamoja na baadhi ya watu watakaoshiriki katika shughuli za kikundi
hicho, ambapo kikao hicho kimehudhuriwa na jumla ya watu 30.
Katika kikao hicho, washiriki wamekubaliana mambo
mbalimbali ya msingi ikiwemo kuanza maandalizi ya kusajili
kikundi cha SHY TALENT FILMS ili kiwe rasmi kisheria na kufanya
kazi zake kwa utaratibu unaotambulika.
Akizungumza katika kikao
hicho, Mkurugenzi wa Misalaba Media, Mapuli Misalaba,
amesema kuanzishwa kwa SHY TALENT FILMS ni sehemu ya dhamira ya taasisi hiyo
kupanua wigo wa kazi zake kwa kugusa moja kwa moja maendeleo ya vijana na jamii
kwa ujumla kupitia sanaa yenye maudhui yenye maana na mwelekeo wa kijamii.
Kwa upande wake, Meneja wa Misalaba Media ambaye pia ni Katibu wa kikundi hicho, Daniel
Sibu, amesema SHY TALENT FILMS itakuwa jukwaa la kujifunza,
kukuza vipaji na kutoa nafasi kwa waigizaji wachanga kushiriki katika kazi za
kitaalamu za filamu na tamthilia, huku akisisitiza nidhamu, mshikamano na ubora
wa kazi.
Naye Mwenyekiti wa SHY TALENT FILMS, Daniel Elimboto, ameeleza
kuwa kikundi hicho kimejipanga kufanya kazi kwa weledi, uwazi na ubunifu,
akisema lengo si burudani pekee bali kuibua vipaji vitakavyoleta mchango chanya
kwa jamii na sekta ya sanaa kwa ujumla.
Aidha, baadhi ya
waigizaji na washiriki waliohudhuria kikao hicho wameishukuru
na kuipongeza Misalaba Media kwa wazo hilo, wakieleza kuwa ni
fursa adhimu ambayo kwa maeneo mengi bado haijakuwepo.
Wamesema hapo awali baadhi yao waliwahi kujiunga na
makundi au vikundi vingine vya maigizo, lakini hawakuweza kuona mafanikio wala
maendeleo ya vipaji vyao, hali iliyowakatisha tamaa.
Hata hivyo, washiriki hao
wameeleza kuwa wana imani na matumaini makubwa
kwa Misalaba Media kutokana na uzoefu wake katika tasnia ya
habari, nidhamu ya kazi na mwelekeo wake wa kuzingatia maendeleo ya vijana na
jamii ambapo wamesema wanaamini kupitia SHY TALENT FILMS, vipaji vyao vitapata
mwelekeo, malezi na fursa za kweli za kujitambua na kufanikiwa.
Misalaba Media kupitia SHY TALENT FILMS inawaomba wadau mbalimbali, wakiwemo taasisi za umma na binafsi,
mashirika yasiyo ya kiserikali, wafanyabiashara, wadau wa sanaa pamoja na watu
binafsi, kujitokeza kuiunga mkono initiative
hii ili kufanikisha malengo yaliyojiwekea.
Ushirikiano huo unaweza kuwa kupitia mafunzo, vifaa,
ufadhili wa miradi ya filamu na tamthilia, au kushirikiana katika kampeni za
kijamii zitakazotumia sanaa kama chombo cha mabadiliko.
Misalaba Media ni chombo
cha habari cha mtandaoni kilichosajiliwa kisheria,
kinachojishughulisha na ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa habari, pamoja
na kuona fursa za kutumia sanaa na ubunifu kama nyenzo ya kuelimisha,
kuhamasisha na kuijenga jamii.
Platform hii si ya burudani tu, bali ni chombo cha
mabadiliko ya jamii, kiwanda cha talanta, na daraja la waigizaji wachanga
kuelekea ndoto zao.
Kwa taarifa zaidi, tembelea ukurasa wetu mpya wa
Instagram: SHY TALENT FILMS
“Kuibua vipaji leo, Kujenga wasanii wa kesho”
Mkurugenzi wa Misalaba Media,
Mapuli Misalaba akizungumza kuhusu dhamira ya Misalaba Media kuanzisha SHY
TALENT FILMS kwa ajili ya kuibua vipaji na kuijenga jamii kupitia sanaa.

Mwenyekiti wa SHY TALENT FILMS, Daniel Elimboto, akizungumza kuhusu malengo ya kikundi na umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha sanaa yenye tija kwa jamii.

Meneja wa Misalaba Media ambaye ndiye Katibu – SHY TALENT FILMS Daniel Sibu akiwaongoza washiriki katika mchezo wa kuamsha mwili na kuburudisha, kabla ya kuendelea na kikao cha kupanga mwelekeo wa SHY TALENT FILMS.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
















Post a Comment