" WANANCHI IGAWILO WAPATA TUMAINI JIPYA BAADA YA ZIARA YA DKT. TULIA

WANANCHI IGAWILO WAPATA TUMAINI JIPYA BAADA YA ZIARA YA DKT. TULIA




Na Lydia Lugakila- Misalaba Media

Mbeya

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, leo Januari 7, 2026, ametembelea Kata ya Igawilo jijini Mbeya kwa lengo la kujionea hali ya daraja lililovunjika katika Mtaa wa Mponja.

Daraja hilo lilikuwa likitumika na Wananchi kama kiunganishi muhimu kati ya mtaa mmoja na mwingine, hivyo kuvunjika kwake kumesababisha adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, ikiwemo kushindwa kupita kwa urahisi kwenda maeneo ya huduma muhimu kama shule, masoko na vituo vya afya.

Akizungumza na wananchi, Dkt. Tulia amesema chanzo cha daraja hilo kuvunjika ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, hali iliyosababisha maji kujaa na kuharibu miundombinu hiyo.

Kufuatia hali hiyo ameahidi kuwa hatua za haraka zitachukuliwa ili kuhakikisha daraja hilo linajengwa upya na kurejesha mawasiliano kwa wananchi.

“Tutahakikisha changamoto hii inatatuliwa kwa haraka ili wananchi waendelee na shughuli zao bila usumbufu,” amesema Dkt. Tulia.

Katika hatua nyingine, Dkt. Tulia amewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka kwenye mifereji ya maji, akieleza kuwa kufanya hivyo kunasababisha mifereji kuziba na hatimaye kuleta madhara makubwa ikiwemo mafuriko na uharibifu wa makazi pamoja na miundombinu.

Aidha, amewataka viongozi wa maeneo mbalimbali kuwa waadilifu katika mipango ya matumizi ya ardhi, kwa kuepuka kuwauzia wananchi maeneo yenye changamoto ya maji kujaa.

“Viongozi acheni kuwauzia watu maeneo yenye changamoto ya mafuriko ili kuepukana na madhara makubwa pindi mvua zinaponyesha,” amesisitiza.

Dkt. Tulia ameeleza kuwa baadhi ya mafuriko yanayosababisha hasara kwa wananchi yanatokana na watu kujenga katika maeneo hatarishi, hali inayozuia mkondo wa asili wa maji na kusababisha maji kutafuta njia mbadala, jambo linaloathiri makazi ya watu.

Ziara hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Kata ya Igawilo, ambao wameeleza imani yao kuwa ahadi hiyo italeta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya daraja na mafuriko katika eneo lao.







Post a Comment

Previous Post Next Post