Na Lydia Lugakila – Misalaba Media
Mbeya
Watanzania wametakiwa kuilinda na kuitunza amani ya Nchi kwa gharama yoyote huku wakisisitizwa kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa CCM Wilaya Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo, wakati akifunga semina ya wenyeviti, makatibu wa UWT Wilaya na madiwani viti maalum kilichofanyika katika ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya.
Akihubiri juu ya umuhimu wa amani, Akyoo,amesema kuwa pindi amani inapopotea hakuna huduma itakayopatikana, watoto hawataweza kusoma na maisha ya kawaida ya wananchi yatasimama kabisa.
“Amani ikishapotea watoto hawawezi kusoma, hospitali hazitafanya kazi, na huduma zote muhimu zitasimama,” alisema Akyoo.
Ameongeza kuwa kila Mwananchi ana wajibu wa kulinda amani ya Nchi, na kuwa siasa za dunia zina uhusiano wa moja kwa moja na uchumi, hivyo nchi inapoingia kwenye migogoro ya ndani, hakuna mwananchi anayekuwa salama.
“Nchi inapoingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe hakuna wa kuuliza huyu ni wa chama gani, watoto wanateseka, hospitali hazifanyi kazi, wagonjwa hawatibiwi, mabomu yanalia kila sehemu na wanawake hujikuta wakikosa msaada,”
Hata hivyo, Katibu huyo amewataka Watanzania kuelewa thamani ya amani na kuepuka kuonja sumu ya machafuko, akisisitiza kuwa amani ni kila kitu katika maisha ya binadamu.
Katika hatua nyingine, Akyoo amewaagiza viongozi wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kuhakikisha wanashughulikia kwa karibu changamoto za vijana, wanawake, wazee pamoja na makundi mengine maalum katika jamii.
Amesema viongozi wana wajibu wa kuwahudumia Wananchi kwa karibu, kuwasikiliza na kushughulikia changamoto zao ili kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
“Viongozi ni lazima muwasikilize Wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa vitendo,” aliongeza kiongozi huyo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment