" Bima ya Afya kwa Wote: CCM imedhamiria Kuwatumikia Wananchi katika haki na usawa

Bima ya Afya kwa Wote: CCM imedhamiria Kuwatumikia Wananchi katika haki na usawa

Na Mwandishi Wetu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, amesema Bima ya Afya kwa wote inatarajiwa kuanza kabla ya mwisho wa Februari 2026. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa haki na usawa kwa Watanzania wote.Mongela ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mashina, katika mji mdogo wa Kagongwa, wilayani Kahama mkoani Shinyanga kuelekea maadhimisho ya miaka 49 ya CCM.Amesema viongozi hao wanayo dhamana kubwa ya Taifa, wakati ambapo Rais Dk Samia Suluhu Hassan anaonyesha dhamira ya wazi ya kuhakikisha Taifa linabaki kwenye umoja na mshikamano."Haki sio vibali tu vya mikutano ya vyama vya siasa, sio kutaka vibali vya kuandamana tu, yote hayo yana msingi, lakini kuna haki ambazo Watanzania wengi wanazililia," amesema Mongela.Amesema kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania, kuwa na jamii yenye ustawi, watu kuwa na uhuru, kuwa na uwezo wa kupata huduma stahiki na bora za afya, kupata huduma za maji safi na salama, huduma za elimu kwa watoto wao, zote ni haki ambazo bila kuwa na amani na utulivu haziwezekani.Mongela amewaelekeza viongozi hao kurudi na kuhamasisha mashina kufanya vikao vya kikatiba ili kuibua changamoto za wananchi wote bila kujali itikadi za vyama, na changamoto hizo zifanyiwe kazi ngazi za kata, wilaya na mkoa ili wananchi wote wapate haki zao."Kufikia mwishoni mwa mwezi Februari, 2026 kila shina na nyumba ya balozi wa shina iwe na bendera, wananchi wawatambue, muwasimamie mabalozi kuitisha vikao vya kikatiba, kwa kuwa ile ndo ngazi ya kusikia changamoto halisi za wananchi wetu na zifanyiwe kazi," amesema Mongela.Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ameahidi kutekeleza yale yote waliyoelekeza ili kuwaletea maendeleo wananchi wote."Sisi tumepokea na tutayafanyia kazi kwa bidii kuwahudumia wananchi wetu, na tutawasimamia kuanzia ngazi ya chini bila kujali itikadi ya vyama, na panapojitokeza changamoto tutazitatua ili kila mmoja apate haki yake. CCM inahudumia watu wote na sio wanachama wake tu," amesema Mlolwa. Mwisho.

Post a Comment

Previous Post Next Post