" WAZIRI ULEGA ACHUKIA  AAGIZA TANROADS KUVUNJA MKATABA NA MKANDARASI BARABARA YA KYERWA–OMRUSHAKA:BILIONI 9 ZIMELIPWA, KAZI ASILIMIA 5 TU.

WAZIRI ULEGA ACHUKIA  AAGIZA TANROADS KUVUNJA MKATABA NA MKANDARASI BARABARA YA KYERWA–OMRUSHAKA:BILIONI 9 ZIMELIPWA, KAZI ASILIMIA 5 TU.

 

Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.

‎Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi imeielekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kagera kufanya taratibu zote za kuvunja mkataba na mkandarasi Shandong Luqiao Co. Ltd, anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa–Omrushaka, kipande cha kilometa 50 kwa kiwango cha lami, ifikapo Februari 28, 2026.

‎Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, Januari 31, 2026, baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo na kubaini hali mbaya ya utekelezaji wake.

‎Uamuzi huo umetokana na kushindwa kwa mkandarasi kutekeleza kazi kwa kiwango kilichokubaliwa, Ikiwa ni miezi  19 imepita tangu kuanza kwa mradi,mkandarasi huyo anatakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ndani ya miezi 36 hadi Juni 2027.

‎Akisoma taarifa ya mradi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Joel Mwambungu, amemueleza Waziri wa Ujenzi pamoja na wananchi wa wilaya ya Kyerwa kuwa mkandarasi huyo amekuwa msumbufu na ameshindwa kufuata maelekezo wanayopewa mara kwa mara.

‎“Tumeitisha vikao mara mbili vya tathmini ya utekelezaji wa mradi huu lakini hajawahi kuhudhuria hata kikao kimoja. Pia tumemuandikia barua aeleze matumizi ya fedha bilioni 9 alizolipwa, lakini hadi sasa hajatoa maelezo yoyote,” amesema Mhandisi Mwambungu.

‎Ameongeza kuwa mkandarasi huyo, licha ya kutumia zaidi ya nusu ya muda wa mkataba, amejikita katika kipande cha kilometa tatu tu kuanzia eneo la Nyakatuntu na lakini hadi sasa amekamilisha asilimia 5.4 pekee ya kazi yote.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa, ameonesha kukerwa na mwenendo wa mkandarasi huyo na kumuomba Waziri wa Ujenzi kuhakikisha hapati tena zabuni nyingine mkoani Kagera, akidai amewavunjia wananchi matumaini yao kwa Serikali.

‎Mapema katikati ya wiki hii, akiwa bungeni, Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Khalid Nsekela, aliuliza swali kuhusu hatma ya barabara hiyo na ni lini Serikali itachukua hatua madhubuti, akieleza kuwa mradi huo umekwama na unaendelea kwa kasi ndogo sana.

‎Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa–Omrushaka unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi bilioni 94.3, ambapo hadi sasa mkandarasi tayari amelipwa shilingi bilioni 9.










Post a Comment

Previous Post Next Post