Fabius Clavery,Misalaba Media-Karagwe, Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, amewasisitiza wananchi wilayani humo kuifanya Bima ya Afya kwa Wote kuwa ajenda ya kila mtu na siyo kuiachia Serikali pekee, akieleza kuwa utekelezaji wake unapaswa kupewa kipaumbele katika kila kaya.
Akizungumza jana Februari 4, 2026 wakati wa mafunzo ya Utawala Bora DC Laizer amesema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu afya bora ni mtaji wa kwanza wa maendeleo, si kwa mtu binafsi tu bali pia kwa jamii kwa ujumla.
DC Laizer ametoa wito huo wakati akihitimisha na kugawa vyeti vya Mafunzo ya Utawala Bora kwa Waheshimiwa Madiwani wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa, mafunzo yaliyodumu kwa siku tatu mfululizo kuanzia Februari 02 hadi 04, 2026, na kufanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe (Angaza).
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, linalolenga kuhakikisha Madiwani nchini kote wanapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kwa kuzingatia sheria na kanuni, ili kufikia uongozi bora na maendeleo endelevu.
Akifafanua zaidi, DC Laizer amesema mara kwa mara Serikali imekuwa ikipokea wananchi wanaohitaji msaada wa matibabu, hali inayolazimu wakati mwingine kutolewa kwa fomu za kuchangisha fedha.
"Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kuathiriwa na gharama kupitia Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote. Niwasihi tuichangamkie fursa hii kwa kupeana elimu juu ya umuhimu wake na kuhakikisha wananchi wanaipokea kwa utekelezaji. Hapo tutakuwa tumejenga jamii yenye afya, uchumi imara na kizazi chenye matumaini,” alisema DC Laizer.
Pia aliwataka viongozi wa vijiji, mitaa, taasisi za dini na makundi ya kijamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya, akisisitiza kuwa bima hiyo ni kinga ya shughuli za kiuchumi kwani maradhi ya ghafla yanaweza kuyumbisha maendeleo ya mtu binafsi na familia endapo hakutakuwa na maandalizi ya awali.
Kwa upande mwingine, Wilaya ya Karagwe tayari imeanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuanza kuwasajili walengwa wa TASAF na wategemezi wao katika ngazi ya kata.
Kata zilizoanza usajili ni pamoja na,Bugene na Chanika,Waliosajiliwa 244 Chonyonyo Waliosajiliwa 177
Kata nyingine zinatarajiwa kufikiwa kulingana na ratiba iliyowekwa. Walengwa wa TASAF wamehimizwa kujitokeza kwa wingi na kwa wakati ili kunufaika na mpango huo.
Ikumbukwe kuwa Serikali imesema itawagharamia wananchi wasio na uwezo wa kuchangia gharama za bima, wakiwemo wazee wasio na kipato, watu wenye ulemavu na kaya maskini kupitia TASAF, ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa huduma za afya kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
Hata hivyo, wananchi wenye uwezo na wasio na bima ya afya wameelekezwa kuchangia kiasi cha shilingi 150,000 kwa kaya ya watu sita (06), hatua inayolenga kuufanya mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote kuwa endelevu na wenye manufaa kwa jamii nzima.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

.jpg)
.jpg)
Post a Comment