WANANCHI wa Kata ya Mzenga na Mafizi wamepongeza hatua ya Mbunge wao, Dkt. Selemani Jafo, kusimamia binafsi ujenzi wa Daraja la Kitomondo hadi usiku, wakisema imeongeza kasi na uwajibikaji kwa mkandarasi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mafizi, mmoja wa wazee wa eneo hilo, Ramadhani Zungwe amesema si jambo la kawaida kwa kiongozi kubaki kijijini hadi usiku akihakikisha kazi inafanyika kama ilivyopangwa.
“Ameonyesha mfano wa kujitoa kwa ajili ya maendeleo yetu. Hii inatupa matumaini mapya,” amesisitiza Zungwe.
Msukumo huo umefuatia maelekezo aliyoyatoa Dkt. Jafo wiki iliyopita kwa mkandarasi, kampuni ya Neloyt Tanzania Limited, akitaka ifikapo tarehe 24 nguzo za daraja hilo ziwe tayari zimemwagwa.
Tangu wakati huo, kazi imekuwa ikiendelea kwa kasi kubwa, huku Dkt. Jafo mwenyewe akishuhudia hatua za ujenzi zinavyopiga hatua.
Naye, Diwani wa Kata ya Mafizi, Mhe. Bora Mayage, amekiri kuwa usimamizi wa karibu wa mbunge huyo umeleta matokeo chanya.
Amesema kasi ya awali ya mkandarasi haikuwa ya kuridhisha, lakini kwa sasa mabadiliko yanaonekana wazi na nguzo za zege tayari zimesimama.
Mbali na hayo, Dkt. Jafo amemtaka mkandarasi kuhakikisha ifikapo Machi 5 zoezi la umwagaji wa slab linakamilika, akiahidi kushiriki pamoja na viongozi wa kata hizo mbili katika hatua hiyo muhimu.
Ameweka bayana kuwa hatokuwa tayari kuona wananchi wake wanaendelea kuteseka wakati Rais, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa pesa ya kukamilisha daraja hilo.
Daraja la Kitomondo linatajwa kuwa kiungo muhimu kwa wakazi wa Mzenga na Mafizi, likirahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi zikiwemo usafiri wa wanafunzi, wafanyabiashara na wagonjwa.
Kukamilika kwake kunatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa maendeleo kwa wananchi wa maeneo hayo.
Post a Comment