" LIGI YA MKOA WA KAGERA YAFIKIA TAMATI, BUHAYA FC YATWAA UBINGWA.

LIGI YA MKOA WA KAGERA YAFIKIA TAMATI, BUHAYA FC YATWAA UBINGWA.


Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.

‎Ligi ya Mkoa wa Kagera msimu wa 2025/26 imehitimishwa rasmi Januari 31, 2026 katika Uwanja wa Kaitaba, Manispaa ya Bukoba, ambapo timu ya Buhaya FC iliibuka mabingwa baada ya kuifunga timu ya Leo Tena kwa bao 1–0 katika mchezo wa fainali.

‎Mashindano hayo yalidhaminiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera yalianza  kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi Desemba 2025 yakiwa na lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya soka mkoani Kagera, sambamba na kuhamasisha wananchi na wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.

‎Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya timu 12 zilizogawanywa katika makundi mawili. Kundi A lilijumuisha timu za Buhaya FC, Hamugembe, Leo Tena, Kaboya, Katoma na Itika FC, huku Kundi B likiwa na timu za Kayanga FC, Karagwe DC FC, Afya FC, Vijana FC, Nkwenda FC pamoja na Greenland FC, ambayo hata hivyo ilijitoa katika mashindano.

‎Timu za Buhaya FC na Leo Tena kutoka Kundi A, pamoja na timu za Afya FC na Kayanga FC kutoka Kundi B, zilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

‎Michezo ya Kundi A ilichezwa katika Kituo cha Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba, huku michezo ya Kundi B ikichezwa katika Kituo cha Karagwe kwenye Uwanja wa Bashingwa.

‎Akizungumza baada ya kutwaa ubingwa huo, Kocha Mkuu wa Buhaya FC, Vicent Mashauri, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri, mshikamano wa wachezaji pamoja na nidhamu ndani ya timu. Ameongeza kuwa ushindi huo umeipa timu morali kubwa ya kujiandaa kwa ajili ya kuuwakilisha Mkoa wa Kagera katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa.

‎“Kwa ujumla ligi ilikuwa ngumu, hasa kutokana na ukweli kwamba tulianza kwa kupoteza mechi mbili za mwanzo kabla ya kushinda michezo iliyofuata. Tunaupongeza uongozi wa Buhaya FC kwa sapoti kubwa waliyoitoa. Wiki ijayo tutaingia kambini kujiandaa kwa ajili ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (ngazi ya kanda), lengo letu likiwa ni kusonga mbele na hatimaye kufuzu kushiriki Ligi Daraja la Pili (First League),” amesema Mashauri.

‎Kwa upande wao, wadau wa michezo mkoani Kagera wamepongeza jitihada za waandaaji pamoja na mdhamini kwa kufanikisha mashindano yaliyoendeshwa kwa mafanikio makubwa, wakieleza kuwa ligi hiyo imekuwa chachu ya kuibua vipaji vipya vya soka na kuimarisha ushiriki wa jamii katika masuala ya maendeleo kupitia ulipaji wa kodi.







  


Post a Comment

Previous Post Next Post