Na: Yusuph Kayanda - KilosaMwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Amani Sewando, ametoa maagizo mazito kwa wataalamu wa Halmashauri kuhakikisha Soko Jipya la Madini la Wilaya linasimamiwa kwa weledi, nidhamu na uwajibikaji ili liwe mkombozi kwa wachimbaji wadogo na kudhibiti utoroshwaji wa madini kiholela.Akizungumza wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi, Sewando alisema kuwa ujenzi wa soko hilo ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha mapato ya Halmashauri na Serikali kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa uwepo wa miundombinu pekee hautoshi bila usimamizi thabiti wa kitaalamu.“Wataalamu simamieni kikamilifu sekta hii, Hakikisheni madini yote yanayochimbwa Kilosa yanapitia katika mfumo rasmi wa mauzo. Hatutaki kuona madini yanatoroshwa na Halmashauri kukosa mapato,” alisisitiza.Aliagiza matumizi ya mifumo ya kidijitali kusajili na kufuatilia mauzo ya madini, akisema hatua hiyo itasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha uwazi katika biashara ya madini.Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uwekezaji Wilaya ya Kilosa, Dinawi Gabriel, alisema maandalizi ya kuanza rasmi kwa shughuli za soko hilo yamekamilika kwa kiasi kikubwa na watahakikisha wafanyabiashara wote wa madini wanazingatia taratibu zilizowekwa.Naye Katibu wa Wachimbaji Wadogo Kilosa, Dodo Sambu, alieleza kuwa kwa muda mrefu wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamikia utoroshwaji wa madini unaowakosesha soko la uhakika na kupunguza kipato chao.Alisema wachimbaji wadogo wamejipanga kuwa mabalozi wa kulinda rasilimali za wilaya kwa kuhakikisha madini yote yanayochimbwa yanauzwa kupitia soko rasmi la Kilosa, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri na kuinua maisha ya wachimbaji.Naye, Diwani wa Kata ya Mbumi, Vitus Kassian, alisema kuanza kwa soko hilo kutachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na kutoa fursa zaidi kwa vijana kujiunga katika shughuli halali za uchimbaji na biashara ya madini.Soko Jipya la Madini la Wilaya ya Kilosa linatarajiwa kuwa kitovu cha biashara ya madini, likileta pamoja wachimbaji, wanunuzi na mamlaka za usimamizi, huku likidhibiti utoroshwaji na kuhakikisha rasilimali za madini zinanufaisha wananchi wa Kilosa na Taifa kwa ujumla.🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


\

Post a Comment