" DC MTATIRO AWAONYA WAZAZI WANAOKATIZA NDOTO ZA ELIMU HASA KWA WATOTO WA KIKE

DC MTATIRO AWAONYA WAZAZI WANAOKATIZA NDOTO ZA ELIMU HASA KWA WATOTO WA KIKE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa watoto wa kike katika safari yao ya elimu, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia mtu yeyote anayekiuka haki ya mtoto kupata elimu.

Mtatiro ametoa kauli hiyo, wakati wa Tamasha la Kitaaluma 2026 ambalo limefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, ambapo walimu na wanafunzi kutoka shule mbalimbali wameshiriki mashindano ya michezo pamoja na utoaji wa tuzo kwa waliofanya vizuri kitaaluma.

Akizungumza katika tamasha hilo, Mtatiro amesema anaendelea kupigania elimu ya mtoto wa kike kwa sababu anaamini ndiyo msingi wa kupata viongozi bora wa baadaye.

Amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi au walezi watakaobainika kuwazuia watoto, hususan wa kike, kuendelea na masomo kwa sababu elimu ndiyo njia ya kuwawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.

Mbali na hilo, Mtatiro aliahidi kuanzisha tamasha la michezo na taaluma kwa walimu pamoja na wanafunzi, na kwamba ahadi hiyo sasa imetekelezwa kwa mafanikio makubwa ambapo amesema ataendelea kuanda matamasha ya michezo kwa ajili ya wanafunzi.

Ameeleza kuwa tamasha hilo limeongeza mshikamano kati ya walimu na wanafunzi, limeimarisha afya kupitia michezo na limewapa nafasi ya kubadilishana uzoefu unaochochea matokeo bora ya kitaaluma.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Manispaa ya Shinyanga, Richard Makoye, amesema tamasha hilo limekuwa sehemu muhimu ya kuunganisha walimu na wanafunzi, kujenga afya, ushirikiano na kuongeza ari ya kujifunza na kufundisha.

Makoye amesema mafanikio hayo yanatokana na mazingira mazuri yanayoendelea kuwekwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, huku akiipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kuendeleza utaratibu huo unaochangia maendeleo ya elimu.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndala, Hamisa Magulu, amesema tamasha hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa limeimarisha mahusiano kati ya shule mbalimbali na kusaidia kupunguza changamoto za afya ya akili kupitia ushiriki wa michezo.

Mmoja wa wanafunzi, Daud Charles wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, amesema michezo hiyo imewajengea afya njema, ushirikiano na kuwatia moyo wa kufanya vizuri zaidi katika masomo.

Katika tamasha hilo kumefanyika mashindano mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, kufukuza kuku, kukimbia na magunia, draft, bao, karata pamoja na michezo mingine ya burudani.

Washindi wa mashindano mbalimbali wamekabidhiwa zawadi, huku walimu na shule zilizofanya vizuri kitaaluma zikitunukiwa vyeti vya pongezi. Katika fainali ya mpira wa miguu, timu ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga iliibuka bingwa baada ya kuifunga timu ya Kidato cha Nne mabao 2-0, na kukabidhiwa kombe, mbuzi watatu pamoja na vinywaji.

Mchezo wa kukimbia kwenye Magunia ukiendelea.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


 

Post a Comment

Previous Post Next Post