Kishapu, Shinyanga
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo limekutana na
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambapo limewasilisha
taarifa ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya umeme na nishati safi,
inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuimarisha Gridi ya
Taifa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Kishapu na Mkoa wa
Shinyanga kwa ujumla.
Katika kikao hicho, TANESCO ilieleza kuwa inaendelea
kutekeleza miradi ya kimkakati katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo Mkoa
wa Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha umeme wa
uhakika kwa maendeleo ya wananchi.
Mradi Mkubwa wa Umeme wa Jua Ngunga Wakaribia
Kukamilika
Moja ya miradi mikubwa iliyowasilishwa ni mradi wa
kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya jua unaotekelezwa katika eneo la Ngunga,
Wilaya ya Kishapu, wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 150.
Mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu
ya kwanza ya Megawati 50 ilianza Desemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Machi
2026 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 323. Hadi sasa, mradi umefikia asilimia
92.6 ya utekelezaji, na hatua za mwisho zinaendelea ili kuanza kuingiza umeme
kwenye Gridi ya Taifa.
TANESCO ilieleza kuwa mradi huu utakuwa na mchango
mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha Gridi ya Taifa na
kuhakikisha Kanda ya Ziwa inapata umeme wa uhakika zaidi.
Upanuzi wa Kituo cha Ibadakuli Kuleta Umeme wa Uhakika
TANESCO pia ilieleza kuhusu mradi wa upanuzi wa Kituo
cha Umeme cha Ibadakuli, ambacho kwa sasa kina uwezo wa Megawati 296.
Kupitia mradi huu, transfoma mpya zinafungwa ili
kuongeza uwezo wa kituo na kuimarisha usambazaji wa umeme. Mradi huu
unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 46.7, na umefikia
asilimia 46.8 ya utekelezaji. Unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.
Mradi huu utasaidia kuondoa changamoto za kukatika kwa
umeme na kufungua fursa mpya za uwekezaji na shughuli za kiuchumi katika
Kishapu na maeneo ya jirani.
Vitongoji 15 Kishapu Vyanufaika na Umeme
Katika hatua nyingine, TANESCO ilieleza kuwa mradi wa
kufikisha umeme katika vitongoji 15 vya Jimbo la Kishapu tayari umeleta matokeo
chanya.
Mkandarasi amekamilisha ujenzi wa miundombinu, ambapo:
Wateja 176 tayari wameunganishwa na umeme
Mradi umetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 11.118
Baadhi ya vitongoji vilivyonufaika ni Buganika
(Idukilo), Itilima, Nzanza, Igalukilo pamoja na vitongoji vingine, jumla vikiwa
15.
Shinyanga Yapata Vitongoji 581 Kupata Umeme
Habari njema zaidi ni kuwa Mkoa wa Shinyanga umepata
mradi mwingine mkubwa wa kufikisha umeme katika vitongoji 581 ndani ya majimbo
mbalimbali.
Mgawanyo wa vitongoji hivyo ni kama ifuatavyo:
Shinyanga Mjini – 20, Itwangi – 63, Solwa – 49, Msalala
– 96, Kahama – 61, Ushetu – 136, Kishapu – 154
Mradi huu tayari mkandarasi amesaini mkataba na
utatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 60, huku TANESCO ikisisitiza kuwa
viongozi wa maeneo husika watashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji.
Madiwani Wakumbushwa Kulinda Miundombinu ya Umeme
Meneja wa Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Hussein Mbulu,
aliwakumbusha madiwani na wananchi kwa ujumla kuwa miundombinu ya TANESCO ni
mali ya umma, hivyo inapaswa kulindwa.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda transfoma na nyaya za
shaba, na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara moja pale vitendo vya
uharibifu vinapotokea.
Nishati Safi ya Kupikia Yapewa Kipaumbele
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Emma
Nyaki, alitumia kikao hicho kutoa elimu juu ya Agenda ya Kitaifa ya Nishati
Safi ya Kupikia, akisisitiza umuhimu wa kuachana na nishati chafu na kuhamia
kwenye matumizi ya majiko janja.
Alieleza kuwa majiko hayo yanaokoa muda, ni salama, na
ni nafuu, ambapo mtu anaweza kupika wali au ugali kwa chini ya unit 350, huku
yakisaidia kulinda afya na mazingira.
Madiwani walionesha kuridhishwa na elimu hiyo na
kukubali kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia katika Jimbo la Kishapu.
Mhandisi mwandamizi wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Anthony Tarimo, akizungumza.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Hussein Mbulu, akizungumza.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Emma Nyaki, akizungumza.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254










Post a Comment