Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK) Bw. Severin Mushi,akizungumza wakati wa mafunzo ya mfumo mpya kwa wafanyabiashara wa Kariakoo.
Na.Mwandishi Wetu- KARIAKOO
Wafanyabiashara wameukubali mfumo wa Usimamizi wa Kodi za ndani (IDRAS) ,huku wakijiandaa kuupokea Jumatatu ya tarehe 9 Februari mwaka huu.
Akizungumza leo 6.2.2026 jijini Dar es salaam katika mafunzo ya mfumo mpya kwa wafanyabiashara wa Kariakoo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK) Bw. Severin Mushi amesema wapo tayari kuanza kuutumia mfumo huo kwa ushirikiano wa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenyekiti huyo amesema kupitia mafunzo ambayo wamepatiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaamini mfumo utakuwa msaada kwao na kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zilikuwepo.
Amesema mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara kwa kuwa yameondoa hofu iliyokuwepo awali na kuwapa uelewa wa pamoja kuhusu matumizi ya mfumo huo.
Bw. Mushi amesema wamejiandaa kuupokea mfumo wa IDRAS, akieleza kuwa jambo lolote jipya huwa linaogopesha kwa wanaolipokea.
Amebainisha kuwa mabadiliko ya kiteknolojia hayaepukiki katika dunia ya sasa, hivyo wafanyabiashara wanapaswa kuendana nayo ili kuboresha ufanisi wa ulipajikodi.
Hata hivyo, Mushi ametoa rai kwa TRA kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutatua changamoto ya mtandao katika baadhi ya maeneo ya biashara, hususani Kariakoo ili kuleta ufanisi wa matumizi mazuri ya mfumo mpya wa IDRAS kwa walipakodi.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kuwa tayari kuupokea mfumo wa IDRAS na kushirikiana na Serikali pamoja na TRA kwa karibu, akisisitiza kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha ulipaji wa kodi unakuwa rahisi na wenye tija.
“Tumejiandaa kuupokea mfumo kuanzia Jumatatu ya tarehe 9 mwezi huu Kikubwa ni kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunalipa kodi na mifumo ya ulipaji iwe rahisi,” amesema Bw. Mushi.
Aidha,Mwenyekiti huyo amependekeza kuwepo kwa kipindi cha mpito cha mafunzo ili kuwapa wafanyabiashara nafasi ya kuuelewa mfumo huo Zaidi na kuleta ufanisi sahihi wa utekelezaji wake.
“Angalau miezi mitatu ya mwanzo iwe ni ya mafunzo na kuwaelimisha watu namna ya kutumia mfumo, watakapokuwa wameuelewa, tutakwenda pamoja,”- Bw. Mushi.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment