Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.
Wananchi wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wanatarajia kunufaika kiuchumi kufuatia kukamilika kwa Daraja la Kamishango, ambalo ni kiunganishi muhimu kwa kata mbalimbali za wilaya hiyo,katika kusafirisha bidhaa, hususan ndizi na mazao mengine ya kilimo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Kenani Kihongosi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Mwambungu, ameeleza kuwa daraja hilo limekamilika kwa asilimia 100 na lipo tayari kuanza kutoa huduma mara tu kazi ndogo zitakapokamilika.
Mhandisi Mwambungu ameeleza kuwa kazi zilizobaki ni pamoja na usimikaji wa taa 56, upakaji rangi kwenye kingo za daraja pamoja na usafishaji wa eneo, akisisitiza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutachochea uchumi wa kata husika na Wilaya ya Muleba kwa ujumla kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao.
Ameongeza kuwa mradi huo umetumia takribani shilingi bilioni 12.5 na kutekelezwa na mkandarasi mzawa, DRK General Merchants Ltd, ukihusisha ujenzi wa daraja pamoja na barabara za maungio zenye urefu wa kilometa 2, utekelezaji wake ulianza Novemba mwaka 2024.
Kwa upande wake, Kenani Kihongosi amepongeza kazi iliyofanywa na mkandarasi pamoja na usimamizi wa TANROADS Mkoa wa Kagera, akimtaka mkandarasi kukamilisha kwa haraka kazi zilizobaki ili daraja hilo lifunguliwe na kuanza kuwahudumia wananchi.
Baadhi ya wananchi, akiwemo Bi. Spenzioza Protazi na Bw. Abdurashid Yunusu, wameishukuru serikali kwa mradi huo wakieleza kuwa hapo awali walikumbwa na changamoto ya usafiri kutokana na daraja la zamani kuwa dogo na kujaa maji wakati wa mvua, huku Daraja la Kamishango likiwa miongoni mwa miradi mitano ya madaraja inayotekelezwa mkoani Kagera kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 45.6 kufuatia athari za mvua za El Niño mwaka 2023.






Post a Comment