" IGP WAMBURA ATOA MAAGIZO KWA KAMISHANA MKAMA

IGP WAMBURA ATOA MAAGIZO KWA KAMISHANA MKAMA







Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, akimvalisha Cheo cha Kamishna wa Polisi (CP) Alex S. Mkama, baada ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kumpandisha cheo kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na kumteua kuwa Kamishna wa Polisi Jamii, hafla ya kumuapisha imefanyika Machi 26,2026 Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam. Picha na Jeshi la Polisi

……….

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura, amemtaka Kamishna wa Polisi Jamii (CP) Alex S. Mkama, kuhakikisha kuwa, anakwenda kusimamia nidhamu na maadili ya Jeshi la Polisi kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari kwa kuwashauri, kuwaelekeza, kuwakemea na kuchukua hatua za haraka kulingana na mahitaji.

IGP Wambura, ameyasema hayo wakati wa hafla ya kumvalisha cheo cha Kamishna wa Polisi CP Alex Mkama baada ya kupandishwa cheo na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na kumteua kuwa Kamishna wa Polisi Jamii, hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam Machi 26,2026.

Kwenye hafla hiyo IGP Wambura ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kuwa, matishio ya uhalifu wa aina zote yanadhibitiwa kikamilifu kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Falsafa ya Polisi Jamii na kuwasimamia Maafisa Polisi Jamii wa Mikoa, Wilaya bila kusahau Polisi Kata/Shehia ambao ndio kiungo muhimu kati ya Jeshi la Polisi na Jamii.

Huku akimtaka kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Polisi Jamii kulingana na uhitaji wa himaya ili kuendelea kusogeza zaidi huduma za Polisi kwa wananchi kwa lengo la kuhakikisha kuwa, uhalifu unaendelea kupungua na kudhibitiwa nchini.

Naye Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Bi. Elizabeth Mapunda, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kusimamia na kuzingatia misingi ya maadili na kuwa mfano kwenye eneo la uongozi kwa kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote atakayethibitika kukiuka maadili.

Akizungumza baada ya kuapishwa kuwa kamishna wa Polisi Jamii CP Alex Mkama, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Pamoja na Menejimenti ya Jeshi la Polisi kwa kupandishwa cheo na kwamba atahakikisha anakwenda kutekeleza majukumu aliyokasimiwa ili kuleta matokeo chanya ikiwemo udhibiti wa vitendo vya kihalifu kwenye jamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post