" KAMATI YA SIASA YA CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAKAGUA MRADI WA MAJI UNAOTEKELEZWA NA SHUWASA KATIKA KATA YA KOLANDOTO

KAMATI YA SIASA YA CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAKAGUA MRADI WA MAJI UNAOTEKELEZWA NA SHUWASA KATIKA KATA YA KOLANDOTO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga ya kukagua miradi ya maendeleo imeendelea, ambapo leo kamati hiyo imetembelea mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) katika Kata ya Kolandoto.

Mradi huo unaotekelezwa kupitia fedha za Wizara ya Maji kutoka Mfuko wa Maji wa Taifa, unahusisha upanuzi wa mtandao wa mabomba ya majisafi katika kata za Kambarage, Ibadakuli, Kizumbi na Kolandoto ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Mhe. Anord Makombe, amesema chama kinaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na fedha za serikali zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Amesema mradi huo wa maji ni muhimu kwa wananchi kwani utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Salum Kitumbo amesema serikali ya Manispaa itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma zinazotolewa.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, amesema serikali inaendelea kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo una lengo la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia huduma muhimu kama maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameipongeza serikali kwa kuleta mradi huo wa majisafi huku wakiomba ukamilike kwa wakati ili uweze kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.

Kwa mujibu wa taarifa ya SHUWASA, ambayo imesomwa na kaimu Mkurugenzi mamlaka hiyo Mhandisi Uswege Musa, mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi katika Manispaa ya Shinyanga ulianza kutekelezwa mwezi Septemba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026.

Mradi huo unahusisha upanuzi wa mtandao wa mabomba ya maji kwa urefu wa kilomita 8.5 kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 119, ambapo unatarajiwa kuwanufaisha takribani wananchi 2,850.

Katika Kata ya Kolandoto, mradi huo umebuniwa kuhudumia maeneo ya Mwanubi na Mwamala, ambapo takribani wananchi 1,749 wanatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kupunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji pamoja na kusaidia kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

kaimu Mkurugenzi mamlaka hiyo Mhandisi Uswege Musa, akizungumza baada ya kusoma taarifa ya mradi huo.Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Makombe, akizungumza  wakati wa ziara ya kukagua mradi wa maji unaotekelezwa na SHUWASA.




Samwel Jackson katibu wa mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini akizungumza wakati wa kukagua mradi wa maji unaotekelezwa na SHUWASA.


 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post