" KAMATI YA UTEKELEZAJI WAZAZI CCM MPANDA YAKAA KIKAO CHA KAWAIDA

KAMATI YA UTEKELEZAJI WAZAZI CCM MPANDA YAKAA KIKAO CHA KAWAIDA

Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mpanda imefanya kikao chake cha kawaida Machi 27, 2026, kikiongozwa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilayani humo, Pius Buzumalle.

Akifungua kikao hicho leo majira ya saa 4:00 asubuhi, Buzumalle aliwataka wajumbe kuwa na umoja, mshikamano na utulivu wakati wa kuchangia ajenda mbalimbali ili kuhakikisha maamuzi yanayofikiwa yanatekelezeka kwa ufanisi.

Katika kikao hicho, wajumbe walielezwa kuwa hali ya uhai wa jumuiya hiyo ni nzuri kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanachama pamoja na mwitikio mzuri wa ulipaji ada. Ilibainishwa kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, zoezi la uandikishaji wanachama wapya limeendelea kushika kasi.

Kwa upande wa miradi, jumuiya hiyo inaendesha shughuli mbalimbali ikiwemo fremu mbili za biashara, shule ya sekondari na ufundi ya Milala pamoja na nyumba ya mtumishi. Ilielezwa kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha shule ya Milala iliyopo katika Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, Manispaa ya Mpanda, inapata hati miliki ya eneo lake.

Aidha, kamati hiyo ilijipanga kufanya maadhimisho ya Wiki ya Wazazi yanayotarajiwa kufanyika Mei 7 hadi 9, 2026, huku ikiahidi kuhakikisha maandalizi yanafanyika kikamilifu ili kufanikisha sherehe hizo.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imepanga kufanya ziara za kitendaji katika kata 27 za wilaya hiyo kwa lengo la kuhamasisha wanachama kujisajili na kulipa ada, pamoja na kutoa elimu na mafunzo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali.

Akizungumzia suala la umoja na mshikamano, wajumbe walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ili kuimarisha jumuiya hiyo na kuhakikisha inatekeleza majukumu yake bila vikwazo.

Kikao hicho kilihitimishwa saa 7:00 mchana, ambapo Mwenyekiti Buzumalle aliwashukuru wajumbe kwa michango yao ya mawazo, ushauri na mapendekezo yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa shughuli za jumuiya hiyo.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Jimotoli Jilala, akizungumza kwenye kikao hicho.

Wajumbe wa kamati ya utekelezaji wazazi CCM wilaya ya Mpanda wakiendelea na kikao cha kawaida kilichofanyika leo Machi 27, 2026.





Post a Comment

Previous Post Next Post