" Maboresho mfumo kodi na maendeleo tuyatakayo

Maboresho mfumo kodi na maendeleo tuyatakayo

Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Misalaba Media Tanga Juhudi za kujiletea maendeleo zinategemea sana ufanisi wa ukusanyaji kodi kutoka kwa wananchi. Wizara, taasisi na vitengo mbalimbali wanaweza wakakaa chini kupanga, kujadili na kuja na mipango mingi mizuri ya maendeleo lakini itakapofika kipengele cha namna ya kutekeleza mipango hiyo, maeneo mengi yatahitaji fedha ili kufanikisha. Kimsingi, kodi ni raslimali muhimu inayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu katika kufikia maendeleo ya kweli yanayohusa maisha ya wananchi kule walipo.Hakuna namna serikali inaweza kuwaletea maendeleo wananchi wake pasipo kukusanya kodi. Kivipi? Mathalani, wananchi wanahitaji kujengewa barabara, madaraja, shule, masoko, hospitali au wanahitaji dawa hospitalini, vitendea kazi katika ofisi za umma na mengine kadha wa kadha; sasa,  ili serikali ifanikishe mahitaji hayo ya wananchi, ni lazima fedha zitumike kununua mahitaji yote muhimu kufanikisha ujenzi na ununuzi wa vifaa mbalimbali, yaani ni hela hapo inahitajika si maneno. Kutokana na umuhimu wa fedha katika kuchochea kasi ya maendeleo, kule kunakokusanywa kodi ni lazima kuangaliwe kwa namna inayostahili ili kama zipo changamoto fulani fulani, basi zifanyiwe kazi na mamlaka husika ili kusiwe na mkwamo katika ukusanyaji wake na bila kuathiri biashara na maisha ya walipakodi kwa jina la kukusanya kodi kwa maendeleo ya nchi. Tunayo Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo yaani 2025-2050. Dira hii ina mwelekeo wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati juu. Tunayo mipango kikubwa katika kila sekta ambayo kwa hakika bila uwepo wa fedha za kutosha, tutaishia kuwa na mipango ya kwenye makaratasi lakini si halisi. Kwa jicho la kuona mbali kuanzia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025-2030 na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan mapema Julai 31, 2024 akaunda Tume ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi. Oktoba 4, 2024, Tume ikaanza kazi rasmi. Lengo ni kuhakikisha kama Taifa tuna uhakika huko tuendako katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa kwa kuzingazia dhamira ya serikali ya kutumia mapato ya ndani (own sources) kugharamia miradi mingi ya maendeleo.Machi 18, 2026, Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Balozi Ombeni Sefue, aliwasilisha ripoti yake mbele ya Rais. Ripoti hiyo ina mapendelezo 284 yenye lengo la kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini. Pamoja na mambo mengine, Tume imependekeza kuimarisha kwa mfumo wa kisera na kisheria ikiwemo kufutwa kwa baadhi ya sheria zilizopitwa ma wakati kama vile sheria ya ushuru wa bidhaa ya sasa baaada ya kutungwa sheria mpya ya ushuru wa bidhaa na huduma. Sanjari na hilo, Tume imependekeza kuondoa utaratibu wa maofisa wa kodi kuonana uso kwa uso na walipa kodi. Kuonana kwa wawili hawa uso kwa uso kunatengeneza mazingira ya kuombana rushwa, na hivyo mlipakodi huumia. Aidha, imependekezwa malipo yafanyike kwa mifumo ya kieletroniki na kuachana na matumizi ya fedha taslimu na nyaraka za karatasi. Balozi Sefue pia ameeleza changamoto ya uwepo wa mamlaka nyingi zinazokusanya kodi. "Hali hii husababisha walipakodi kutozwa ada na ushuru mara kwa mara katika chanzo kimoja, jambo linaloongeza gharama na usumbufu na hata kuchochea vitendo vya rushwa," amesema.Mambo ni mengi katika taarifa hiyo kama nilivyoeleza hapo juu kuwa Tume imependekeza mambo 284 ya kufanyiwa kazi na serikali kwa mustakabali mwema wa ulipajikodi na kwa maendeleo endelevu. Ni kiu ya serikali na wananchi kwa ujumla kuona nchi yetu inapiga hatua kubwa za kimaendeleo. Hatuna namna nyingine zaidi ya kulipa kodi, jambo zuri ni kuwa Tume imeshauri pia wigo wa walipakodi uongezeke ili tuwe na kundi kubwa la walipakodi badala ya kuwa na walipakodi wachache wanaoumia katika kulijenga Taifa letu. Taifa hili ni letu sote, hivyo tushiriki pamoja katika ujenzi wake kwa kulipa kodi kikamilifu kwa moyo wa uzalendo na upendo mwingi. Maendeleo tuyatakayo yanahitaji raslimalifedha kupitia kodi, hivyo basi, tulipe kodi kama tunayataka maendeleo ya kweli.

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post