" Video: POLISI WAKAMATA MASHINE BANDIA 60 ZA KUBAHATISHA, RAIA WA KIKEGENI ASHIKILIWA

Video: POLISI WAKAMATA MASHINE BANDIA 60 ZA KUBAHATISHA, RAIA WA KIKEGENI ASHIKILIWA

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limetoa taarifa ya kukamatwa kwa mashine bandia 60 za michezo ya kubahatisha pamoja na kumshikilia raia wa kigeni aitwaye Wang Renbiao (28) kwa tuhuma zinazohusiana na tukio hilo. Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chilya, amesema kuwa operesheni hiyo ilifanyika Machi 24, 2026 majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Mkuzo, Manispaa ya Songea. Amesema mtuhumiwa alikamatwa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, maafisa wa michezo ya kubahatisha pamoja na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akiwa amehifadhi mashine hizo kwenye stoo kwa lengo la kuzisambaza katika maeneo mbalimbali ya starehe vijijini wilayani Mbinga. Kwa mujibu wa Kamanda Chilya, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mashine hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu. Aidha, mtuhumiwa alikutwa na risiti feki pamoja na stika za kampuni ya Cleopatra Gaming Tanzania Ltd ambazo zilionekana kughushiwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa huo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa tisa tarehe Machi 25, 2026, wanaohusishwa na matukio ya unyang’anyi na wizi wa pikipiki katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo. Majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi. Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika. Kamanda Chilya ametoa onyo kali kwa wahalifu akisisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma si mahali salama kwa vitendo vya uhalifu, na kuwataka kujihusisha na shughuli halali. Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post