Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi, anatarajiwa kuwasili mkoani Shinyanga
tarehe 4 Machi 2026 kwa ziara ya kikazi ya siku nne itakayohitimishwa tarehe 7
Machi 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Siasa,
Itikadi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Richard Raphael Masele, wakati
akizungumza na MISALABA MEDIA, ziara hiyo inalenga kuimarisha uhai wa chama,
kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na kusikiliza na kutatua kero
za wananchi.
Katika ziara hiyo, Ndugu Kihongosi atatembelea mabalozi na
wenyeviti wa mashina katika ngazi mbalimbali na kushiriki mikutano ya ndani kwa
lengo la kukagua na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya shina hadi
wilaya.
Siku ya kwanza, Machi 4, ataanza ziara yake katika mji wa
Isaka kwa kukagua mradi wa bandari ya nchi kavu, kisha kuelekea Kahama kukagua
ujenzi wa standi kubwa ya mabasi ya kisasa katika Manispaa hiyo.
Baada ya ukaguzi wa miradi, atafanya mkutano wa hadhara
utakaofanyika katika Uwanja wa Phantom mjini Kahama kuanzia saa nane mchana
hadi saa kumi na mbili jioni ambapo wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi
kushiriki mkutano huo na kuwasilisha kero na changamoto zao ili zipatiwe
ufumbuzi.
Tarehe 5 Machi 2026, Katibu huyo atafanya ziara katika Jimbo
la Ushetu ambapo atakagua miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa umeme wa REA
uliopo Kisuke pamoja na daraja la Ubagwe.
Mchana atafanya kikao na mabalozi, na baadaye kuanzia saa
nane hadi saa kumi na moja na nusu jioni, atafanya mkutano wa hadhara katika
Kata ya Ulewe ambapo wananchi wa jimbo la Ushetu wameaswa kujitokeza kwa wingi
ili kuwasilisha changamoto zao.
Tarehe 6 Machi 2026, ziara itaendelea katika Manispaa ya
Shinyanga ambapo atatembelea mradi wa ujenzi wa standi ya kisasa ya mabasi ya
Mkoa pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga uliopo Kata ya Ibadakuli.
Baada ya mikutano ya ndani na mabalozi, atafanya mkutano wa
hadhara katika Uwanja wa Shule ya Msingi Town kuanzia saa nane mchana hadi saa
kumi na mbili jioni ambapo wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kusikiliza
na kuwasilisha kero zao.
Ziara hiyo itahitimishwa tarehe 7 Machi 2026 katika Wilaya
ya Kishapu ambapo kuanzia saa mbili asubuhi atazungumza na wananchi katika eneo
la Maganzo.
Aidha, katika mikutano yake ya hadhara ataeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana
chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kimetoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ili kusikiliza maelezo ya kiongozi huyo pamoja na kuwasilisha changamoto zao kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment