" SERIKALI, SEKTA BINAFSI KUIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA KUCHOCHEA AJIRA NCHINI

SERIKALI, SEKTA BINAFSI KUIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA KUCHOCHEA AJIRA NCHINI






Na Abduly Iddy, Dar es Salaam

Serikali imesema ushirikiano kati yake na Sekta binafsi utaendelea kuwa chachu muhimu ya kuimarisha huduma za afya nchini, hususan katika kuboresha huduma za dharura kupitia mpango wa kuanzisha uzalishaji wa magari ya wagonjwa (ambulance) mkoani Tanga.

Akizungumza Machi 5, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao cha maandalizi ya kuanzisha uzalishaji wa magari hayo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe.Batilda Burian, amesema Serikali inakaribisha uwekezaji huo unaofanywa kwa kushirikiana na SO Company Limited kwani utaimarisha upatikanaji wa huduma za dharura za afya nchini hususan magari ya wagonjwa.

Amesema uzalishaji wa ambulance ndani ya nchi utaongeza upatikanaji wa magari ya kisasa ya kuwahudumia wagonjwa na kupunguza muda wa kuwafikia wananchi wanaohitaji msaada wa haraka wa kitabibu, hatua itakayosaidia kuokoa maisha ya watu.

“Mradi huu ni hatua muhimu tunapoimarisha mfumo wetu wa huduma za afya. Kupatikana kwa ambulance zinazozalishwa hapa nchini kutarahisisha usambazaji wake katika maeneo mbalimbali, hususan ya pembezoni,” amesema, RC Batlida.

Aidha, amesema mradi huo pia utaleta manufaa ya kiuchumi kwa kufungua fursa za ajira kwa vijana, kukuza wazalishaji wa ndani wa vipuri na kuchochea maendeleo ya sekta zinazohusiana na uzalishaji wa vifaa vya magari na huduma za afya.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya sekta ya afya pamoja na uchumi wa taifa.

Mradi huo unatarajiwa kuimarisha huduma za dharura za afya huku ukifungua fursa mpya za ajira na maendeleo ya kiuchumi nchini.

  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post