" SABABU ZA SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI

SABABU ZA SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI






Na Mwandishi wa OMH

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) leo, Machi 5, 2026, imesema Serikali iliamua kushirikiana na sekta binafsi katika uendeshaji wa baadhi ya mashirika ili kuongeza ufanisi, mtaji na matumizi ya teknolojia katika kuendeleza uchumi wa nchi.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara kutoka OMH, Lightness Mauki, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha ufanisi wa mashirika pamoja na kuvutia uwekezaji.

Bi. Mauki alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kipindi cha Kumekucha kinachorushwa na ITV Tanzania, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi za kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, unaotarajiwa kufanyika Machi 16 hadi 18 mwaka huu katika ukumbi wa PAPU Tower, Arusha.

Akifafanua historia ya uamuzi wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi, alisema miaka ya nyuma Serikali ilikuwa na zaidi ya mashirika ya umma 400, lakini baadaye iliamua kuuza baadhi yake kwa sekta binafsi na kubaki na machache ambayo inamiliki hisa chache.

“Yalikuwa zaidi ya mashirika 400. Tuliamua kuuza baadhi kwa sekta binafsi na kubaki na kampuni 56 ambazo tuna hisa chache,” alisema Bi. Mauki.

Aliongeza: Tuli ‘offload’ hisa ili sekta binafsi ichukue hisa nyingi zaidi, hatua ambayo inatuwezesha kushirikiana katika ujuzi, mtaji na teknolojia na kuhakikisha kampuni hizo ziendelee kukua.”

Aidha, ushirikiano huo una manufaa kwa pande zote mbili: sekta binafsi inapata fursa ya kuwekeza na kupata faida, huku Serikali ikipata gawio na kuhakikisha uwekezaji unawanufaisha wananchi.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, gawio kutoka kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache limeongezeka kwa asilimia 357, kutoka Sh58.26 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia Sh266.52 bilioni mwaka 2024, ikionesha ukuaji mkubwa na mafanikio ya mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi.

Bi. Mauki alisema kuwa katika kipindi hicho hicho, uwekezaji wa Serikali katika kampuni ambazo inamiliki hisa chache uliongezeka kwa asilimia 140, ukipanda kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh3.6 trilioni, jambo linaloashiria ukuaji endelevu na ufanisi wa mkakati wa kushirikiana na sekta binafsi.

Akijibu swali la mtangazaji kuhusu nani anaweka nia ya kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji wa kampuni hizo, Bi. Mauki alisema hatua hiyo ilikuwa ni mkakati wa Serikali wenye lengo la kuimarisha ufanisi katika mashirika ya umma.

“Serikali iliona mashirika ni mengi na wakati huo huo teknolojia inakua kwa kasi na mahitaji ya mtaji ni makubwa, hivyo kulikuwa na haja ya kufanya kazi na sekta binafsi ili tuweze kushirikiana katika uendeshaji wa mashirika hayo,” alisema.

Alifafanua kuwa mkakati huo ulilenga kuhakikisha Serikali inaendelea kubaki na hisa katika kampuni za kimkakati huku ikitoa nafasi kwa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji.

“Ulikuwa ni mkakati mahususi wa Serikali kuhakikisha tunagawanya hisa na tunabaki nazo chache kwenye mashirika na kampuni za kimkakati,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali haiwezi kuacha umiliki wote kwa sababu ina wajibu kwa umma.

“Huwezi kutoa asilimia 100 kwa sababu Serikali ina wajibu kwa umma kuhakikisha wananchi wanapata huduma na bidhaa mbalimbali,” alisema.

Kuhusu ushiriki wa vijana katika uwekezaji huo, Bi. Mauki alisema Serikali imeandaa mkakati mpya kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mpango wa muda mrefu wa miaka 25 wa OMH utakaonza kutumika Julai 1, 2026.

Alisema mpango huo utapanua wigo wa kampuni na taasisi zitakazoingizwa kwenye soko la hisa ili kuwapa wananchi wengi zaidi, hususan vijana, nafasi ya kumiliki hisa na kupata gawio.

“Kuna mkakati ambao tumeuweka kupitia Dira ya Taifa 2050 pamoja na mpango wetu wa miaka 25 ambao utaanza Julai 1, 2025. Tutapanua wigo wa kampuni na taasisi tunazozileta kwenye soko la hisa pamoja na kuongeza ushiriki wa vijana,” alisema.

Aliongeza kuwa eneo la ushiriki wa vijana halikuguswa kwa kiwango kikubwa katika mpango unaoisha Juni 30 mwaka huu, lakini katika mpango mpya wa muda mrefu litapewa kipaumbele zaidi.

  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post