Na Lydia Lugakila-Misalaba Media
Mbeya.
Wafanyabiashara Mkoani Mbeya wameendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa na elimu inayotolewa na taasisi ya MoWi Consulting, hususan kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa kodi (IDRAS) pamoja na mbinu bora za kuendesha biashara kwa ufanisi na kuepuka hasara.
Akizungumza baada ya kushiriki semina hiyo, Bw. Joas Sanga, ambaye ni mtumishi kutoka Kanisa la Uinjilisti Mbalizi Mkoani Mbeya na anayehusika na shughuli za biashara za taasisi ya kanisa hilo, amesema kuwa wamepata maarifa muhimu yatakayowasaidia kusimamia vyema shughuli zao mbalimbali za kijamii zikiwemo shule, hospitali, gereji na hoteli.
Sanga amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, wamejifunza namna bora ya kudhibiti na kusimamia biashara zao, hususan katika utunzaji sahihi wa kumbukumbu za kifedha.
Ameongeza kuwa pia wamepata uelewa kuhusu mbinu za kuwavutia na kuwahudumia wateja, jambo ambalo litasaidia biashara zao kukua na kudumu kwa muda mrefu.
“Nawashukuru sana MoWi Consulting natamani semina hizi ziendelee kufanyika mara kwa mara na tunawaahidi kuwa sisi wafanyabiashara tutakuwa tayari kushiriki kila tutakapopata nafasi, kwa sababu mafunzo haya yana umuhimu mkubwa kwetu,” amesema Sanga.
Aidha, amebainisha kuwa kupitia mfumo wa IDRAS wamegundua umuhimu wa kurasimisha biashara zao kupitia vyombo vya Serikali ili ziweze kudumu na kukua.
Ameongeza kuwa kabla ya semina hiyo alikuwa na uelewa mdogo, akiamini kuwa masuala ya mifumo ya biashara yanahusisha zaidi watu wenye elimu ya juu pekee.
Kwa upande wake, Stewart Asajile maarufu kama “Mbeya Boy”, kijana mbunifu kutoka Soweto na mfanyabiashara anayejihusisha na shughuli mbalimbali pamoja na mbunifu wa nembo ya Mkoa wa Mbeya, ameipongeza MoWi Consulting kwa mafunzo hayo.
Asajile ameongeza kuwa kabla ya semina hiyo alikuwa akifanya baadhi ya mambo kimakosa, ikiwemo kuajiri marafiki zake bila utaratibu rasmi, hali iliyosababisha kupoteza muda na fedha kutokana na kukosekana kwa uwajibikaji.
Kijana huyo amesema kuwa kwa sasa amejifunza umuhimu wa kufanya biashara kwa kuzingatia mahitaji ya soko, kuepuka kufanya maamuzi kwa mihemko, na kuchagua bidhaa zinazohitajika kwa wakati husika ili kuepuka hasara.
Mbali na hilo, amesema kuwa amekuwa akijitahidi kuwaandaa vijana katika masuala mbalimbali ya maendeleo, akibainisha kuwa hata katika familia nyingi, vijana hawapati elimu ya kutosha kuhusu masuala ya biashara.
Semina hiyo imeandaliwa na MoWi Consulting na kufanyika katika Ukumbi wa Eden, jijini Mbeya, ikiwa imewakutanisha wafanyabiashara wa kada mbalimbali, wakiwemo wadogo, wa kati na wakubwa, pamoja na mameneja, wamiliki wa biashara na wahasibu.
Aidha akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa MoWi School of Business, Willa John Tinga, amesema kuwa wafanyabiashara wengi huanzisha mifumo katika biashara zao lakini mifumo hiyo hushindwa kudumu kutokana na kutokuzingatia mazingira halisi ya biashara husika.
Tinga amesisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni muhimu katika uendeshaji wa biashara, zikiwemo uidhinishaji wa michakato, utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu, ukaguzi na uhakiki, ulinzi wa mali, pamoja na usimamizi na ufuatiliaji endelevu.
Amewahimiza wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa na utaratibu rasmi wa kutunza taarifa za mapato, na kwamba taarifa hizo ziwekwe kwa wakati mara tu baada ya muamala kukamilika.
Nao baadhi ya washiriki wa semina hiyo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa ya kipekee na yenye manufaa makubwa, yakilenga kutoa uelewa wa kina kuhusu mfumo wa IDRAS ambao tayari umeanza kutumika, pamoja na kuwajengea uwezo wa kubuni na kuimarisha mifumo ya ndani ya biashara zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MoWi Consulting, CPA Baraka Mori, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa semina zilizopita, bado kuna wafanyabiashara wengi hawakupata fursa ya kushiriki na kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa IDRAS Februari 9, 2026, baadhi ya wafanyabiashara wamekumbana na changamoto mbalimbali, hivyo semina hiyo iliyofanyika imelenga kutoa ufumbuzi wa changamoto hizo.
“Semina ya awali iliwakusanya watu wengi sana na muda haukutosha kugusa kila eneo wakati huo mfumo ulikuwa bado haujaanza kutumika kikamilifu" alisema Mori.
"Sasa mfumo umeanza kufanya kazi, hivyo tunawasaidia washiriki kuelewa kwa vitendo na namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo,” amesema Mori.
Ameongeza kuwa matumizi ya mfumo wa IDRAS yataleta unafuu mkubwa katika uendeshaji wa biashara kwa kuongeza usahihi, uwazi na ufanisi, hivyo kuwasaidia wafanyabiashara kuendesha shughuli zao bila usumbufu.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254








Post a Comment