" ZIARA YA MAGANYA YAKAGUA MRADI WA MAJI SONGEA

ZIARA YA MAGANYA YAKAGUA MRADI WA MAJI SONGEA


Na osama Mohamedi, Misalaba Media -Ruvuma Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Ndugu Maganya Fadhiri Rajabu, amefanya ziara ya kukagua mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa na SOUWASA katika Manispaa ya Songea,  Mkoani Ruvuma leo Machi 30, 2026. Ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo muhimu unaotarajiwa kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa, amesema mradi wa maji Songea ni sehemu ya mpango wa Serikali ya kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika miji 28 nchini. Ameeleza kuwa mkataba wa mradi huo ulisainiwa Machi 10, 2022 kati ya Wizara ya Maji na mkandarasi wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), huku utekelezaji wake ukianza Januari 2, 2024 na kufikia asilimia 6.5 hadi sasa.Kibasa amefafanua kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 145.77 unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo kidaka maji katika mto Njuga, mtambo wa kisasa wa kuchuja na kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 16 kwa siku, pamoja na matanki matatu ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa lita milioni 9 kwa jumla. Pia, unahusisha ujenzi wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza maji yenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 na ukarabati wa mtambo wa Matogoro.Aidha, ameainisha kuwa baadhi ya kazi zilizokwisha kufanyika ni pamoja na usanifu wa miundombinu, ujenzi wa matanki mawili katika maeneo ya Maji Wilaya na Chandamali, na ujenzi unaoendelea wa tanki la Mahilo ambalo limefikia asilimia 70. Pamoja na mafanikio hayo, Kibasa ametaja changamoto ya kubadilika kwa chanzo cha maji kutoka bwawa lililopangwa awali hadi mto, kutokana na sababu za kiufundi, jambo lililoathiri kasi ya utekelezaji wa mradi.Kwa upande wake, Maganya amesisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na subira na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akieleza kuwa juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeendelea kuleta maboresho katika sekta ya maji nchini. Wananchi wa Mahilo, akiwemo Abubakary Kawelea, Casian Luoga na Maria Ndunguru, wameipongeza Serikali kwa mradi huo na kuomba mkandarasi kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kuondoa kabisa changamoto ya maji katika Manispaa ya Songea.



Post a Comment

Previous Post Next Post