" MWANAMKE AUAWA KATIKA MAZINGIRA YA UTATA, POLISI SHINYANGA WAMSAKA MTUHUMIWA

MWANAMKE AUAWA KATIKA MAZINGIRA YA UTATA, POLISI SHINYANGA WAMSAKA MTUHUMIWA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Songambele, Kata ya Salawe, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukutwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Taarifa za tukio hilo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele, Razaro Enock, ambaye amesema tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Machongo ambapo marehemu alikutwa akiwa amefariki huku chanzo cha kifo hicho kikibaki kuwa kitendawili katika hatua za awali.

“Yule mama alifariki katika mazingira ya kutatanisha, mwili wake ulikuwa na majeraha. Inasemekana alikuwa na mgogoro na mume wake, ambaye hakuwepo nyumbani. Aidha, alidaiwa kuishi na mwanaume mwingine aliyemtambulisha kama kaka yake, lakini baadaye ilibainika kuwa si ndugu yake bali alikuwa na uhusiano wa kimapenzi naye,” amesema Enock.

Ameongeza kuwa, baada ya muda mfupi wa kuishi pamoja, wawili hao walitofautiana na mwanaume huyo kuondoka na mali zake, na muda mfupi baadaye ndipo tukio hilo la kifo lilipotokea.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, watoto wa marehemu walidai kuwa siku ya tukio mwanaume huyo alifika usiku na kuwahamasisha watoto kulala mapema, jambo linalozua hisia kuwa huenda akawa na uhusika katika tukio hilo.

Akizungumza na Misalaba Media, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amesema tukio hilo limethibitishwa kutokea Machi 23, 2026 majira ya saa moja asubuhi.

Amesema marehemu aliyetambulika kwa jina la Mariam Cosmas Mafumba mwenye umri wa Miaka 40, alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake huku uchunguzi wa awali ukionyesha kuwa alipigwa kwa kitu kigumu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani.

“Upelelezi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa wa tukio hilo anasadikika kuwa ni mume wake, Manyanda Mbuye, ambaye baada ya tukio alitoroka. Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili achukuliwe hatua za kisheria,” amesema SACP Magomi,.

Aidha, ameeleza kuwa chanzo kinachodhaniwa kusababisha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, ambapo mtuhumiwa alimshuku marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.

Kamanda huyo amelilaani tukio hilo akisema ni la kikatili na lisilokubalika katika jamii, huku akisisitiza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha mtuhumiwa anapatikana na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Nitoe wito kwa wanandoa na wanaoishi pamoja kuzingatia upendo, kuvumiliana na kutafuta suluhu ya migogoro yao kwa njia ya amani. Kitendo cha kuua ni kosa la jinai na hakikubaliki,” amesema SACP Magomi,.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa tukio hilo huku likiwahimiza wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa.

  SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post