" KONGOLE NECTA KWA MPANGO WA KUPANDA MITI 150,000 KUTUNZA MAZINGIRA

KONGOLE NECTA KWA MPANGO WA KUPANDA MITI 150,000 KUTUNZA MAZINGIRA


Na Dk. Reubeni Lumbagala, misalaba media.

Utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mtu bila kujali umri, jinsia au kiwango cha elimu. Iwe ni mtoto, kijana, mtu mzima au mzee, kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi mazingira. Faida za utunzaji mazingira zinawanufaisha wote, huku madhara ya uharibifu wake yakiwaathiri wananchi kwa ujumla. Hivyo, ni muhimu mikakati madhubuti ya uhifadhi mazingira ikawekwa na kutekelezwa mapema.

Kwa sasa, dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, hali inayolazimu nchi mbalimbali kuweka mikakati ya kukabiliana nayo ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa maisha ya sasa na vizazi vijavyo. Tanzania nayo imeathirika na hali hiyo, na hivyo Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuhamasisha upandaji miti kwa watu binafsi, taasisi, makampuni na wizara.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza utunzaji wa mazingira. Tangu akiwa Makamu wa Rais hadi sasa akiwa Rais, ameendelea kutoa msukumo mkubwa wa kupanda miti na kulinda uoto wa asili. Hata katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa Januari 27, 2026, alitumia fursa hiyo kupanda miti na kusisitiza umuhimu wa kurejesha uoto wa asili uliopotea.

Katika kuunga mkono juhudi hizo za Serikali, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, limeanzisha mpango wa kupanda miti 150,000 katika taasisi mbalimbali za elimu nchini, ikiwemo shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Machi 18, 2026, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, alizindua rasmi zoezi hilo katika Shule ya Sekondari Makutupora jijini Dodoma, ambapo miti 600 ilipandwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Prof. Said alisema mpango huo unatokana na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya NECTA yaliyofanyika Desemba 16, 2023. Alieleza kuwa, kutokana na NECTA kuwa miongoni mwa watumiaji wakubwa wa karatasi zinazotokana na miti, taasisi hiyo ina wajibu wa kurejesha mazingira kwa kupanda miti kama sehemu ya mchango wake katika uhifadhi wa mazingira.

Mpango huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuboresha mandhari katika taasisi za elimu. Uwepo wa miti shuleni na vyuoni utaongeza uzuri wa mazingira na kuleta hali rafiki kwa ufundishaji na ujifunzaji.

Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, NECTA ilipanda miti 82,676, huku mwaka 2024/2025 idadi hiyo ikiongezeka hadi miti 110,400. Kwa mwaka 2025/2026, taasisi hiyo imejiwekea lengo la kupanda miti 150,000. Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yatategemea zaidi utunzaji wa miti hiyo baada ya kupandwa ili kuhakikisha inaleta manufaa endelevu.

Kwa ujumla, juhudi za NECTA zinastahili kupongezwa kwa kuwa ni mchango muhimu katika kulinda mazingira na kujenga taifa lenye uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo ya sasa na baadaye.

Post a Comment

Previous Post Next Post