Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Dkt. Charles Kitima, Askofu Mfumbusa amefariki dunia leo Jumanne tarehe 14,Aprili, 2026, majira ya saa 11:45 Alfajiri, wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma, alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura.
Kwa mujibu wa Vatican News, Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Jumatano ya Aprili 22, 2026, jimboni Kondoa.
Itakumbukwa kwamba Aprili 9, 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa amemteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa, Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication (CEPACS),” kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasilianiano ya Jamii.
Aidha, mtandao wa kijamii wa Vatican umebainisha kwamba Kanisa limempoteza Askofu na mtaalam mbobezi wa Mawasiliano ya Jamii.
Hayati Askofu Mfumbusa alizaliwa tarehe Mosi Aprili 1962 mjini Kondoa na ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64.
Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Juni 1992 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Askofu Matthias Joseph Isuja, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI (Hayati) Machi 12, 2011 akaanzisha Jimbo Katoliki la Kondoa, na kumteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa kuwa Askofu wake wa kwanza, na hivyo kuwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mei 15, 2011, akisaidiana na Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza wakati huo pamoja na Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp., wa Jimbo Katoliki la Zanzibar.
Askofu Bernardin Mfumbusa amefariki dunia akiwa amelitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 33, na kama Askofu mwenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa miaka 14.
Mungu ailaze mahali pema Mbinguni roho ya marehemu Askofu Mfumbusa...Amina
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment