" Hamu ya Maridhiano: Viongozi wa Dini na Wanasiasa Wahimiza Amani Baada ya Ripoti

Hamu ya Maridhiano: Viongozi wa Dini na Wanasiasa Wahimiza Amani Baada ya Ripoti

  

Viongozi wa dini na wanasiasa nchini wametoa mwito wa dhati kwa Watanzania kudumisha amani, utulivu, na mshikamano kufuatia kukamilika na kuwasilishwa kwa ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Ripoti hiyo inawasilishwa leo Aprili 23,2026.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Alhad Mussa Salum, amesisitiza kuwa huu ni wakati wa kujenga imani miongoni mwa wananchi na kuamini uwezo wa ndani katika kutatua changamoto za kitaifa bila kutegemea msaada wa nje. 

Salum amebainisha kuwa tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, ina wajumbe wenye weledi mkubwa, hivyo ni muhimu ripoti hiyo ipokewe, ichambuliwe, na iwapo kutakuwa na upungufu, mifumo iliyopo itumike kurekebisha badala ya kujenga chuki.

Kiongozi huyo wa JMAT ameongeza kuwa kutokuaminiana kati ya wananchi na viongozi wao kunaweza kukwamisha juhudi za kujitawala, akionya kuwa matukio ya Oktoba 29 ya mwaka jana yanapaswa kuwa chachu ya kujenga taifa imara zaidi badala ya kurudia makosa yaliyopita. 

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kanisa la Evangelical Fellowship Church Tanzania (EFCT), Askofu Charles Howard, ameeleza hamu yake ya kuiona Tanzania inayojenga misingi ya kusikilizana na kuridhiana hata pale kunapokuwa na tofauti za kifikra. Amesema misingi ya dini zote inahimiza amani na kuheshimiana, hivyo Watanzania hawana budi kutumia maadili hayo kuimarisha umoja wa kitaifa.

Naye Askofu Godfrey Songambele wa Kanisa la Tumaini la Mataifa Yote (HOFAN), amekumbusha kuwa amani ya kweli inapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa haki kwa wananchi, akisisitiza kuwa "amani ni wimbo, lakini haki ni matendo." 

Mtazamo huu wa hitaji la haki na maridhiano umeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Hassan Doyo, ambaye amesema mustakabali wa Tanzania unategemea wanasiasa wanaoweza kukaa pamoja na kujadili maendeleo, uchumi, na usalama wa nchi. Doyo ametoa mwito kwa wananchi kutokubali kushawishiwa kufanya vurugu na viongozi wa kisiasa, badala yake walinde tunu ya amani iliyopo.

Katika kutoa mwelekeo wa kisiasa, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amebainisha matarajio yake kuwa ripoti hiyo itasema ukweli mtupu kuhusu nini hasa kilisababisha uvunjifu wa amani uliotokea wakati wa mchakato wa uchaguzi. Maoni haya ya viongozi mbalimbali yanadhihirisha kiu ya Watanzania kuona taifa linasonga mbele kwa masikilizano na kurejea katika hali ya utulivu wa kudumu baada ya taarifa hiyo ya tume ya uchunguzi kuwekwa wazi kwa umma.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post