" MAWAKALA WA CRDB BENKI WAWAFIKIA WANANCHI SHINYANGA KUPITIA KAMPENI YA “BONGE LA WAKALA”

MAWAKALA WA CRDB BENKI WAWAFIKIA WANANCHI SHINYANGA KUPITIA KAMPENI YA “BONGE LA WAKALA”


Baada ya uzinduzi wa kampeni ya “Bonge la Wakala” uliofanyika katika Tawi la Benki ya CRDB Shinyanga, mawakala wa benki hiyo wameanza kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kuwapatia elimu ya huduma za kifedha na namna ya kunufaika na fursa zilizopo kupitia kampeni hiyo.

Mawakala hao wametembelea maeneo mbalimbali ya biashara na makazi ikiwemo Soko la Nguzonane, Soko la Kambarage, Lubaga, Soko Kuu la Shinyanga, Stendi ya Mkoa (Manyoni), Kitangili maeneo ya mashine za kukoboa mpunga, Stendi ya Zamani pamoja na mitaa mbalimbali ya Ngokolo.

Katika ziara hiyo, wananchi walipata nafasi ya kufahamishwa kuhusu huduma zinazotolewa kupitia CRDB Wakala, faida za kufanya miamala ya kibenki karibu na maeneo yao pamoja na fursa za kushiriki kampeni ya “Bonge la Wakala” inayotoa zawadi mbalimbali kwa mawakala na wateja wa benki hiyo.

Akizungumza wakati wa shughuli hizo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza matumizi ya huduma za mawakala, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma za kibenki kwa urahisi zaidi.

Amesema mawakala wameendelea kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa huduma za kifedha kwa kuwafikishia wananchi huduma karibu na maeneo yao, hali inayosaidia kupunguza msongamano katika matawi ya benki na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wakati.

Mbali na utoaji wa elimu, shughuli hizo zilipambwa na burudani kutoka kikundi cha Kambi ya Nyani, ambacho kilitoa burudani katika kila eneo lililotembelewa na kuvutia wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na mawakala wa CRDB.

Wananchi waliopata elimu hiyo wameeleza kufurahishwa na hatua ya benki hiyo kusogeza huduma na elimu ya kifedha karibu nao, huku wakiahidi kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa kupitia kampeni ya “Bonge la Wakala”.

Kampeni hiyo inaendelea katika maeneo mbalimbali ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, kuongeza matumizi ya huduma za kidigitali na kuhamasisha ukuaji wa biashara za mawakala wa CRDB nchini.

Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Bonge la Wakala uliofanyika leo Juni 25, 2026 mjini Shinyanga. 

Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Bonge la Wakala uliofanyika leo Juni 25, 2026 mjini Shinyanga. 





 

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post