" JKCI KINARA AFRIKA MASHARIKI, YAFANYA UPASUAJI ZAIDI YA 3,000 WA MOYO KWA MWAKA

JKCI KINARA AFRIKA MASHARIKI, YAFANYA UPASUAJI ZAIDI YA 3,000 WA MOYO KWA MWAKA



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Miradi ya Maendeleo na Fursa za Vijana kwa Mwaka 2025/26 katika Ukumbi wa Habari MAELEZO ulipo Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Jijini Dodoma.

Na. Meleka Kulwa, Dodoma

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuongoza katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jangwa la Sahara, ikifanya zaidi ya upasuaji 3,000 wa tundu dogo kwa mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge, amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya pamoja na kuimarika kwa rasilimali watu, vifaa tiba na miundombinu ya kisasa.

ameyabainisha hayo Aprili 9,2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma, Aidha, Dkt. Kisenge amesema kuwa JKCI iliyoanzishwa mwaka 2015 kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa bobezi, kufanya tafiti na kutoa mafunzo, imefanikiwa kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo zinapatikana ndani ya nchi, hatua iliyopunguza utegemezi wa kwenda nje ya nchi kwa matibabu hayo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya moyo yanaongoza kwa kusababisha vifo duniani, yakigharimu maisha ya takribani watu milioni 17.9 kila mwaka, huku asilimia 75 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Pia ameongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizoanzisha hospitali maalum za matibabu ya moyo kutokana na uwekezaji mkubwa unaohitajika katika sekta hiyo.

Amesema kuwa JKCI hufanya zaidi ya upasuaji 3,000 wa tundu dogo kwa mwaka pamoja na zaidi ya upasuaji mkubwa 800 wa kufungua kifua, huku pia ikifanya upasuaji tata kama TAVI pamoja na upasuaji maalum kwa watoto ikiwemo Ozaki na Truncus.

Aidha, amebainisha kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kuwa kituo cha utalii wa matibabu, ambapo wagonjwa kutoka ndani na nje ya Afrika wanakuja kupata huduma katika taasisi hiyo.Ameongeza kuwa katika kusogeza huduma karibu na wananchi, JKCI imeanzisha matawi sita katika maeneo ya Tazara (Temeke), Kawe, Oysterbay, Kariakoo, Chato na Arusha, hali iliyoongeza idadi ya wagonjwa kutoka wastani wa 400 kwa siku mwaka 2022 hadi zaidi ya 1,100 mwaka 2025.

Pia ameongeza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuongeza huduma za upasuaji kwa watoto kupitia ufadhili wa Serikali na wadau mbalimbali, ambapo mamia ya watoto wamefanyiwa upasuaji bila malipo.

Aidha, amebainisha kuwa JKCI imeendelea kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo mfumo wa DOZEE kwa ajili ya ufuatiliaji wa wagonjwa pamoja na mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao uliosaidia kupunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo imeanza mchakato wa kuanzisha huduma za upandikizaji wa moyo, huku ikilenga kuanza rasmi huduma hiyo ifikapo mwaka 2030.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali imewekeza maabara ya kisasa inayotumia teknolojia ya akili mnemba na roboti, hatua iliyopunguza muda wa majibu ya vipimo kutoka saa tatu hadi saa moja.

Pia ameongeza kuwa JKCI imeendelea kuvutia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali, huku pia ikiingia makubaliano ya kushirikiana na mataifa ya Afrika katika utoaji wa huduma na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa afya.Amesema kuwa taasisi hiyo imeanzisha mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo (CardioTan) unaowakutanisha wataalamu kutoka zaidi ya nchi 40 duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na mbinu za kisasa za matibabu.

Aidha, amebainisha kuwa kupitia huduma za tiba mkoba, JKCI imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 35,000 katika mikoa mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa katika mwaka 2025 pekee, taasisi hiyo ilitoa huduma kwa wagonjwa 252,915 huku wagonjwa 2,710 wakifanyiwa upasuaji, wakiwemo 836 waliopata upasuaji mkubwa wa moyo.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post