Na Lydia Lugakila-Misalaba media
Mbeya
“Huduma hii itakushawishi uje Tanzania mara kwa mara… tumekuwa kama tupo nyumbani.”
Hayo ni maneno ya baadhi ya waimbaji wa kwaya kutoka Chingola, Nchini Zambia, waliotembelea Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) linaloongozwa na mtumishi wa Mungu, Mchungaji Thobias Tambikeni, kwa ajili ya kuhudumu kupitia uimbaji.
Wakizungumza baada ya ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kanisani hapo Aprili 3, na kuongozwa na mhubiri kutoka Zambia, Askofu Winner Simbeye wa kanisa la Ancient of Days Assemblies of God walisema wameguswa sana na huduma ya kanisa hilo.
Walibainisha kuwa wamejifunza mambo mengi ya kiroho watakayoyapeleka nchini kwao ili kuleta mabadiliko chanya katika makanisa yao.
Beatrice Banda Kalunga kutoka kwaya ya wanawake Zambia alisema hii ni mara yake ya pili kufika kanisani hapo, na amefurahishwa sana na huduma, umoja, pamoja na mshikamano wa wanawake katika shughuli za kanisa.
Alieleza kuwa wamebarikiwa sana na uzoefu huo na kwamba utawavutia kurejea Tanzania mara kwa mara.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa wanawake wa kanisa la Ancient of Days Assemblies of God Zambia, Catherine Mumba, alisema pia hii ni ziara yake ya pili nchini Tanzanianambapo amesifia mapokezi mazuri waliyopewa na Mchungaji Tambikeni pamoja na waumini wake, akieleza kuwa walipokelewa kwa upendo na urafiki mkubwa.
Aliongeza kuwa walifurahishwa na idadi kubwa ya waimbaji na ubora wa huduma ya uimbaji, na kwamba watakaporejea Zambia watashiriki yale mema waliyojifunza.
Pia aligusia unyenyekevu wa viongozi wa kanisa hilo, akisema hawajikwezi kwa nafasi zao bali wanamtumikia Mungu kwa unyenyekevu mkubwa.
“Natarajia tukirudi tena Tanzania, hasa hapa Forest ya Kwanza, tutaona mambo mapya zaidi.
"Nimevutiwa sana na huduma ya vijana; wana shauku na furaha kubwa katika kumtumikia Mungu,” alisema Mumba.
Aidha, alimshukuru Mchungaji Tambikeni kwa ukarimu wake na moyo wa kiungu aliouonesha kwa wageni wao.
Naye Aizak Simbeye, mwalimu wa shule ya Jumapili kutoka Zambia, alisema kanisa hilo lina kwaya zenye nguvu ya Mungu na kuwa, japokuwa kuna msemo “nyumbani ni nyumbani,” wao wameona Tanzania kuwa zaidi ya nyumbani.
Kwa upande wake, Josephine Nkole, kiongozi wa masuala ya muziki katika kwaya hiyo, alisema amefurahishwa na namna kwaya zilivyokuwa zikiimba kwa umoja na ustadi.
Bi Nkole Alibainisha kuwa si rahisi kuwakusanya watu katika vikundi vya kwaya bila neema ya Mungu, huku akimpongeza Mchungaji Tambikeni kwa hekima yake katika uongozi.
Matobwe Judithi Kolala naye alisema amevutiwa na ushiriki wa vijana katika vikundi vya wanawake kanisani hapo, na akaahidi kuwahamasisha vijana wa Zambia kujiunga na huduma kama hizo ili kujifunza maadili mema ya kiroho.
Katika ibada hiyo ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika katika kanisa la TAG Forest ya Kwanza, Mchungaji Thobias Tambikeni alisema kuwa kati ya Ijumaa kuu zote zilizowahi kupita, ya mwaka huu imekuwa ya kipekee kwa namna ilivyowagusa waumini na kuwatoa katika vifungo vya kiroho.
Mchungaji Tambikeni Aliwasisitiza waumini kujiepusha na dhambi, akieleza kuwa dhambi huwatoa wanadamu katika utukufu wa Mungu.
“Tutakwenda mbinguni, tutakutana na ndugu zetu, tutavaa miili isiyoharibika na kumshangilia Yesu wetu. Lakini ni lazima tujilinde dhidi ya dhambi,” alisema.
Aliongeza kuwa kila muumini anapaswa kupinga dhambi, hasa zile za aibu kama uasherati, uchafu, uadui, uchawi, uzinzi, wizi, fitina na masengenyo" alisema Mchungaji Tambikeni.
Akihubiri, Askofu Winner Simbeye wa kanisa la Ancient Of Days Assemblies Of God alisisitiza umuhimu wa waumini kubaki kanisani hata baada ya kuimba, badala ya kuondoka mapema.
Askofu Simbeye Alifananisha hali hiyo na kuacha sahani ya chakula, akieleza kuwa neno la Mungu ndilo humfanya mtu akutane na Mungu kikamilifu.
“Tunapoimba na kusifu, tubaki hadi mwisho ili tukutane na Yesu na aliteswa kwa ajili yetu, alipigwa na kudhalilishwa kwa ajili ya ukombozi wetu, hivyo ni muhimu tukumbuke mateso yake na kuacha dhambi,” alisema.
Aliongeza kuwa mateso ya Yesu yalikuwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu, hivyo waumini wanapaswa kuishi maisha matakatifu na kuepuka dhambi, kwani kufanya hivyo ni kama kumrudisha tena Yesu msalabani.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment