" MKUSANYA MAPATO BUMBULI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI

MKUSANYA MAPATO BUMBULI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI






Na Mwandishi Wetu, Lushoto

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, imemfikisha Mahakamani Mkusanya Mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Bw. Haji Issa Mdoe, kwa tuhuma za rushwa na uhujumu uchumi.

Mshtakiwa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Lushoto katika kesi ya uhujumu uchumi namba 6647/2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Rose Ngoka.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Bw. Haji Issa Mdoe anakabiliwa na makosa mawili ya wizi akiwa mtumishi wa umma, kinyume na kifungu cha 258(1), 265 na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Aidha, anakabiliwa pia na shtaka la kuisababishia serikali hasara, kinyume na aya ya 10(1) na (4) ya jedwali la kwanza, zikisomwa pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 marejeo ya mwaka 2022.

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bw. John Chihangala, alidai kuwa kati ya Mei 21, 2020 na Novemba 16, 2021, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli wilayani Lushoto, mshtakiwa akiwa katika nafasi yake ya Mkusanya Mapato, aliiba fedha kiasi cha shilingi 1,584,600 mali ya halmashauri hiyo.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi huku akijua ni kinyume na sheria, na hivyo kuisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka yote yanayomkabili mahakamani hapo.

Mahakama ilimruhusu mshtakiwa kuwa nje kwa dhamana huku taratibu za kisheria zikiendelea.

Post a Comment

Previous Post Next Post