" MWANACHADEMA BRUCE NYAMWANGI ATOA UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA ZILIZOSAMBAA MTANDAONI

MWANACHADEMA BRUCE NYAMWANGI ATOA UFAFANUZI KUHUSU TUHUMA ZILIZOSAMBAA MTANDAONI







NA DENIS MLOWE IRINGA

MWANACHAMA hai wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bruce Nyamwangi, amezungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa kueleza ukweli kuhusu madai yaliyosambazwa mitandaoni na mwanachama mwenzake, Hilda Newton.

Bruce amesema kuwa usiku wa jana alipata usumbufu mkubwa kupitia simu yake kufuatia taarifa zilizosambazwa mtandaoni zikimtaja yeye pamoja na mwanachama mwenzake, Daniel Naftali, kuwa wapo mkoani Arusha kwenye kambi inayodaiwa kutumika kufanya ushawishi, kurubuni viongozi wa chama na kuwaandalia simulizi zinazodai kuwa chama kinaenda kufutwa.

Amesema kuwa taarifa hizo zimeleta taharuki kubwa, si tu kwa wanachama, bali pia kwa familia na watu wanaomfahamu, hivyo kulazimika kuweka wazi ukweli.

Amesisitiza kuwa kwa zaidi ya wiki mbili amekuwa mkoani Iringa, ambako ni nyumbani kwao, kutokana na shughuli za kifamilia za kimila kama kusafisha makaburi.

Bruce amesema kuwa hata viongozi na wanachama wa CHADEMA waliopo Iringa wanaweza kuthibitisha uwepo wake mkoani humo.

Ametaja pia kuwa tarehe 28 au 29 ya mwezi uliopita, Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa alifanya ziara Iringa kutembelea familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Iringa, marehemu Frank John Nyalusi, na Bruce alikuwepo kwenye ziara hiyo amesema pia muda mfupi baadaye alikutana na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Iringa, William Mungai, kwenye eneo la Kalenga Hotel kwa zaidi ya saa tano.

Aidha, Bruce ameeleza kuwa alikuwepo kwenye msiba wa aliyekuwa Waziri, William Lukuvi, akisema kuwa hata waandishi wa habari waliokuwepo wanaweza kuthibitisha hayo.

Ameelezea masikitiko yake juu ya tabia ya baadhi ya watu kukurupuka na kusambaza taarifa zisizo na msingi, akisema hali hiyo inachafua taswira ya chama na kuumiza watu wasiokuwa na hatia.

Bruce amesema kuwa kama kiongozi wa chama, ana wajibu wa kuzingatia kanuni, maadili na katiba ya chama inayohusu maadili ya viongozi na wanachama.

Amefafanua kuwa hadi sasa hajawahi kupokea barua yoyote ya kutenguliwa katika nafasi yake, hivyo bado ni Mwenyekiti wa Kamati ya mwenezi wa Kanda ya Nyasa na pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Kanda.

Ameeleza kuwa anaifahamu Kanda ya Nyasa kwa undani, ikiwa na majimbo 31 pamoja na kata zaidi ya 120, na kwamba chama katika kanda hiyo kipo imara kikisubiri kipyenga cha kuendelea na shughuli za kisiasa. Hata hivyo, amesema kumeibuka mtindo wa watu kujipanga katika makundi yanayojiona kama “watoto pendwa”, jambo linalovuruga umoja na mshikamano wa chama.

Bruce amebainisha kuwa anaunga mkono hatua yoyote ya chama kuchunguza tuhuma, lakini ametaka hatua zichukuliwe pia kwa watu wanaotunga au kusambaza tuhuma zisizo za kweli.

Amehoji faida ya vita ya ndani badala ya kuunganisha nguvu kupambana na chama tawala.

Amesema kuwa yeye ni mwanachama mwaminifu wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka 17 tangu aanze siasa zake, na hajawahi kuwa mwanachama wa chama kingine.

Amesema kuwa anaendelea kutekeleza majukumu yake kama kiongozi mpaka pale taratibu za chama zitakapomtaka vinginevyo. Bruce amesema hawezi kujiuzulu kwa shinikizo la maneno bali atasubiri maelekezo rasmi kutoka kwa viongozi wakuu wa chama.


Pia amesisitiza kuwa hana mpango wa kufungua kesi mahakamani, akisema mahakama si sehemu ya kutatua mgogoro huu, bali taratibu za chama ndizo zifuatwe.

Kuhusu madai kuwa ana uhusiano wa karibu na mtu anayejulikana kama Salim Asas, Bruce amesema uhusiano wao ni wa kifamilia na upo kwa muda mrefu, hauhusiani na siasa au masuala ya chama. Ameeleza kuwa Asas alikuwa na ukaribu na baba yake mdogo ambaye ndiye mlezi wake.

Bruce amemalizia kwa kusema kuwa tabia ya kusambaza taarifa za kupotosha inapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa sababu inavunja misingi ya chama.

Amesema kuwa tayari ameshapeleka barua kwa Katibu Mkuu wa chama kuomba hatua zichukuliwe ili kuzuia mashambulizi ya aina hiyo dhidi yake. Amehitimisha kuwa ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa CHADEMA na yuko tayari kufuata maelekezo yoyote yatakayotolewa na chama

Post a Comment

Previous Post Next Post