" TAARIFA ILIYOTUFIKIA MUDA HUU KUTOKA JESHI LA POLISI

TAARIFA ILIYOTUFIKIA MUDA HUU KUTOKA JESHI LA POLISI














TAARIFA KWA UMMA

Jeshi la Polisi linaendelea na majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria na kutokana na ushirikiano wa wananchi na wadau wengine katika kubaini na kuzuia uhalifu hali ya usalama nchini ni shwari.

Wiki hii waumini wa dini ya kikristo wameingia katika kipindi ambacho watahitimisha mfungo wa Kwaresma ambapo utafuatiwa na Sikukuu za Pasaka. Ukamilishaji huo wa mfungo wa kwaresma na kuanza kwa sikukuu hizo za Pasaka huambatana na ibada za mchana na nyingine hufanyika usiku.

Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuanzia ngazi ya Kata na tutashirikiana na kamati za usalama katika nyumba za ibada kuhakikisha wakati wote hasa wa ibada zitakazo fanyika usiku usalama unakuwepo wa kutosha ili watakao kwenda kushiriki waweze kushiriki na kurudi majumbani salama.

Pamoja na hakikisho hilo, Jeshi la Polisi lingependa kutoa wito kwa kila mmoja wetu wakati wa ibada na sherehe hizo za Pasaka tunapotoka majumbani mwetu tuhakikishe makazi yetu tunaacha uangalizi kwa ajili ya usalama.

Aidha, kama tutaruhusu watoto wetu kutoka kwa ajili ya kwenda kusheherekea sikukuu maeneo stahiki na salama kila mmoja ahakikishe wanakuwa na uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu.

Pia, tunatoa wito kila mmoja wetu kuzingatia sheria, kanuni na ishara za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazo tokana au zinazo sababishwa na uzembe pamoja na kuendesha chombo cha moto katika hali ya ulevi.

Aidha, tukumbuke kuchukuwa tahadhari kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha tuache na tujiepushe na tabia za kupita sehemu ambazo maji mengi yametuama au yanayotiririka na inaonekana wazi ni hatari kuvuka.

Tunarudia tena kutoa tahadhari hii kwasababu tumeshuhudia baadhi ya Watanzania wenzetu wakipoteza maisha walipojaribu kuvuka sehemu hatarishi ambazo zimejaa maji na yanayotiririka wengine walikuwa wanatembea kwa miguu na baadhi wakiendesha vyombo vya moto.

Tumeshuhudia pia watoto waliopoteza maisha kutokana na kusombwa na maji na wengine kutumbukia kwenye mashimo yaliyo chimbwa na kuachwa wazi. Wazazi/walezi wanapewa tahadhari kuwalinda watoto dhidi ya madhara kama hayo na wale waliochimba mashimo na kuyaacha wazi wayafunike au wayafukie kuepusha madhara kwa watoto.

Imetolewa na;
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma, Tanzania
www.polisi.go.tz

Post a Comment

Previous Post Next Post