" NYOKA ALIYEKUWA AKIFUGWA AUAWA BAADA YA KULETA TAHARUKI MAVIMBA

NYOKA ALIYEKUWA AKIFUGWA AUAWA BAADA YA KULETA TAHARUKI MAVIMBA






Mkaguzi wa Kata ya Milola, Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/INSP) Aloyce Andrew, kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo, wamefanikiwa kumuua nyoka aliyekuwa akifugwa ambaye alisababisha taharuki kwa wakazi wa eneo la Mavimba, njia panda ya mnadani na wananchi wengine kushindwa kuendelea na shughuli zao kutokana na hofu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi waliomuarifu mkaguzi huyo kuhusu uwepo wa mwananchi anayefuga nyoka, bila kufahamika anamtumia kwa madhumuni gani, jambo lililozua hofu kubwa miongoni mwao huku wengjne wakishindwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Katika tukio hilo Mkaguzi huyo amewataka wananchi kuepuka kujihusisha na imani potofu ambazo mara nyingi zimekuwa chanzo cha kuvuruga amani na utulivu katika jamii huku akimtaka mwananchi huyo kuacha mara moja vitendo hivyo ambavyo vinaleta taharuki katika jamii.

Aidha, amesisitiza kuwa imani hizo potofu huchangia kudidimiza maendeleo, akitoa mfano wa tukio hilo ambapo ufugaji wa nyoka ulisababisha hofu kwa wananchi wanaojishughulisha na shughuli zao za kiuchumi.

Vilevile, amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu au viashiria vyake, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Post a Comment

Previous Post Next Post