Na Mapuli Kitina Misalaba
Viongozi wa Seneti wa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa
Shinyanga wameendelea na ziara yao ya kutembelea vyuo takribani 17 mkoani humo,
ambapo leo wametembelea Chuo cha St. Joseph kilichopo mjini Shinyanga na
kuzungumza na wanachuo pamoja na kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya
kijamii, uongozi na maadili.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Seneti Mkoa
wa Shinyanga, Lukomanga Jinyage, amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ya nchi,
akieleza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya taifa na ustawi wa vizazi
vijavyo.
“Tambueni kuwa amani ya nchi yenu ni
hazina kubwa. Hakuna mtu kutoka nje atakayekuja kuilinda kwa niaba yenu. Ni
wajibu wetu sote kuhakikisha tunailinda na kuidumisha kwa manufaa ya sasa na ya
baadaye,” amesema Jinyage.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuwa makini na kauli
au ushawishi wowote unaoweza kuvuruga amani, akiwataka kutumia busara na
kuchukua nafasi yao katika kuijenga jamii yenye mshikamano.
Kwa upande wake, Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa wa
Shinyanga, Sharon Callist Mathias, amewahamasisha wanachuo kujitambua na
kutumia vyema muda wao chuoni kwa kujifunza, kushiriki shughuli za maendeleo na
kujenga uwezo wa kujiajiri.
“Chuo siyo tu sehemu ya kupata elimu ya
darasani, bali ni mahali pa kujijenga kitabia, kiakili na kiuongozi. Jitahidini
kutumia muda wenu vizuri, jengeni nidhamu na epukeni vishawishi vinavyoweza
kuharibu ndoto zenu,” amesema Sharon.
Naye Katibu wa Seneti Wilaya ya Shinyanga Mjini,
Samwel Samson, amewataka wanafunzi kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya,
makundi yasiyofaa na tabia zisizokubalika kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa
nidhamu na bidii katika masomo.
“Maisha ya chuo yanahitaji umakini mkubwa.
Epukeni mambo yanayoweza kuharibu mustakabali wenu, zingatieni masomo, na
jengeni misingi imara ya maisha yenu ya baadaye,”
amesema Samson.
Katika ziara hiyo, viongozi hao pia wamesimamia
uchaguzi wa viongozi wa Seneti tawi la Chuo cha St. Joseph, ambapo nafasi
mbalimbali ikiwemo mwenyekiti na katibu zilijazwa. Baada ya kupatikana kwa
viongozi hao, wamewataka kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na
kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Viongozi waliochaguliwa wameeleza utayari wao wa
kushirikiana na wanachuo wenzao pamoja na Seneti ya Mkoa katika kuimarisha
uongozi na kushughulikia changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Baada ya hafla hiyo, viongozi wa Seneti Mkoa wa
Shinyanga walipata fursa ya kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo cha St.
Joseph Kampasi ya Shinyanga, Pili Sizya Makalanga, ambapo walijadiliana masuala
mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanachuo, uimarishaji wa uongozi wa
wanafunzi pamoja na ushirikiano kati ya Seneti na uongozi wa chuo.
Katika mazungumzo hayo, viongozi wa Seneti wameeleza
dhamira yao ya kuhakikisha wanachuo wanapata mazingira bora ya kujifunza na
kushiriki kikamilifu katika shughuli za uongozi kupitia Seneti, huku
wakisisitiza umuhimu wa taasisi za elimu kuendelea kushirikiana na vyombo vya
wanafunzi ili kukuza nidhamu, uwajibikaji na maendeleo ya vijana.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Pili Sizya
Makalanga, amepongeza Seneti kwa ziara hiyo, akieleza kuwa imekuwa na mchango
mkubwa katika kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala ya uongozi na
kuwahamasisha kushiriki katika maendeleo ya chuo na jamii kwa ujumla. Aidha, ameahidi
kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa chuo na Seneti ili kuhakikisha
malengo ya kuwajenga vijana yanatimia.
Ziara ya viongozi wa seneti Mkoa wa Shinyanga inaendelea katika vyuo vingine mkoani Shinyanga, ikiwa na lengo la kufikia vyuo vyote 17, ambapo Seneti inalenga kuimarisha uongozi wa wanafunzi, kutoa elimu na kuhamasisha maendeleo ya vijana wa vyuo.
Viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga wakizungumza na wanachuo wa St. Joseph, wakitoa elimu kuhusu fursa za ajira, uongozi na masuala ya jamii.
Katibu wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Lukomanga Jinyage akieleza
umuhimu wa kulinda amani na mshikamano kwa maendeleo ya vijana na taifa kwa
ujumla.
Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Sharon Callist Mathias akihamasisha wanachuo kushiriki kikamilifu katika uongozi na shughuli za maendeleo.

Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Sharon
Callist Mathias akihamasisha wanachuo kushiriki kikamilifu katika uongozi na
shughuli za maendeleo.

Katibu wa Seneti Wilaya ya Shinyanga Mjini, Samwel Samson akizungumza na wanachuo, akisisitiza nidhamu, bidii katika masomo na kujiepusha na makundi yasiyofaa.


Wanachuo wa St. Joseph wakifuatilia kwa makini hotuba za viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 22, 2026.

Wanachuo wa St. Joseph wakifuatilia kwa makini hotuba
za viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 22, 2026.

Wanachuo wa St. Joseph wakifuatilia kwa makini hotuba
za viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 22, 2026.
Viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga wakiwa katika kikao na Makamu Mkuu wa Chuo cha St. Joseph Kampasi ya Shinyanga, wakijadili maendeleo ya wanachuo na ushirikiano wa taasisi.
Viongozi wa Seneti wakifanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo cha St. Joseph kuhusu fursa na changamoto zinazowakabili wanachuo.
Picha ya pamoja baada ya mazungumzo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

















Post a Comment