" SERIKALI KUTOA AJIRA 45,000, MAGEUZI MAKUBWA MFUMO WA UTUMISHI 2026/27 YAJA

SERIKALI KUTOA AJIRA 45,000, MAGEUZI MAKUBWA MFUMO WA UTUMISHI 2026/27 YAJA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeweka bayana mpango wake kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikilenga kuimarisha ufanisi, uwazi na utoaji wa huduma bora katika Utumishi wa Umma.

Hayo yamesemwa leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Amesema Katika mpango huo, kipaumbele kikubwa kimewekwa kwenye ajira ambapo jumla ya nafasi 45,000 za ajira mpya zinatarajiwa kushughulikiwa ili kujaza mapengo katika taasisi mbalimbali za umma. Sambamba na hilo, vibali vya ajira mbadala 7,124 vitatolewa ili kuhakikisha utendaji kazi hauathiriki pale watumishi wanapoondoka kazini.

"Serikali  imepanga kuhakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi katika taasisi 425 pamoja na kushughulikia madai ya waliostaafu au waliokoma utumishi kutoka kwa waajiri 200. Aidha, usimamizi wa malipo ya mishahara utaimarishwa kwa taasisi 510 ili kuhakikisha haki na stahiki za watumishi zinalipwa kwa wakati."amesema Mhe.Ridhiwani

Aidha amesema kuwa Katika kuboresha mifumo ya kiutumishi, uhakiki wa watumishi (staff audit) utafanyika katika taasisi 127 zinazotumia mfumo wa e-Watumishi, huku taasisi 35 ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo huo zitawezeshwa kujiunga nao. Mfumo huo pia utaendelea kuhuishwa kwa kuongeza huduma mtandao, kuboresha teknolojia na kuunganisha na mifumo mingine ya Serikali na sekta binafsi.

Hatua nyingine muhimu ni kuandaliwa kwa “dashboard” maalum itakayowezesha upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka mifumo mbalimbali kama e-Watumishi, e-Msawazo, e-Utendaji na Watumishi Portal, kwa ajili ya kusaidia maamuzi ya kiutendaji katika ngazi mbalimbali.

Katika kuimarisha usimamizi wa rasilimaliwatu, Serikali imepanga kufanya uchambuzi wa utofauti wa mishahara ili kuishauri kuhusu namna bora ya kuoanisha viwango vya mishahara kwa muda wa kati na mrefu. Pia, vikao vya Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara pamoja na mabaraza ya majadiliano vitaendelea kuratibiwa.

Kwa upande wa utawala bora, kampeni za maadili zitatekelezwa katika mikoa miwili na halmashauri 30, huku malalamiko 3,500 ya kiutumishi yakitarajiwa kushughulikiwa ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazingatiwa.

Serikali pia imepanga kuhamisha watumishi 7,000 na kujaza nafasi 500 za uongozi ili kuimarisha utendaji katika taasisi za umma. Aidha, mafunzo ya mifumo ya kidijitali kama e-Mrejesho yataendelea kutolewa, pamoja na kusakinishwa kwa “Shared Government Contact Center” katika taasisi 20 za umma.

Katika eneo la sera na miongozo, Serikali itakamilisha mapitio ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma na Sera ya Menejimenti na Ajira ya mwaka 2008 ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Pia, miongozo mbalimbali itaboreshwa ili kuimarisha miundo, utoaji huduma na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Kwa upande wa ustawi wa watumishi, juhudi zitaelekezwa katika kuimarisha ujumuishwaji wa makundi mbalimbali mahali pa kazi pamoja na kukamilisha mwongozo wa kudhibiti changamoto za afya ikiwemo VVU/UKIMWI, magonjwa yasiyoambukiza na afya ya akili.

Vilevile, Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo Klabu ya Viongozi jijini Dodoma pamoja na nyumba ya kiongozi wa kitaifa mstaafu, sambamba na kuendelea kutoa huduma kwa viongozi wa kitaifa wastaafu 21 kwa mujibu wa sheria.

Kwa ujumla, mpango huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia, usimamizi bora wa rasilimaliwatu na utoaji wa huduma zinazokidhi matarajio ya wananchi.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post