Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeweka bayana mikakati yake kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikilenga kuongeza ufanisi katika kudhibiti na kuzuia vitendo vya rushwa nchini kwa kutumia mbinu za kisasa na ushirikishwaji mpana wa jamii.
Hayo yamesemwa leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Waziri Ridhiwani amesema kuwa TAKUKURU imepanga kufanya utafiti wa kitaifa wa hali ya utawala na rushwa nchini (NGACS), ambao unatarajiwa kutoa tathmini ya kina kuhusu viwango vya rushwa pamoja na kupima mafanikio ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na tatizo hilo.
Katika kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma, taasisi hiyo itaendelea kuimarisha usimamizi wa fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inazingatiwa na kuondoa mianya ya ubadhirifu.
Sambamba na hilo, TAKUKURU itaendeleza uchunguzi wa tuhuma za rushwa zilizopo pamoja na kushughulikia kesi mpya zitakazojitokeza, huku mashauri hayo yakiendelea kuendeshwa mahakamani kwa mujibu wa sheria kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka.
Katika kuendana na maendeleo ya teknolojia, TAKUKURU imepanga kusakinisha kituo cha kisasa cha kuhifadhi taarifa (data centre) katika jengo jipya la Makao Makuu, pamoja na kukamilisha na kuanza kutumia mfumo wa takwimu na uchunguzi utakaorahisisha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za rushwa.
Aidha, taasisi hiyo itaendelea kutekeleza mpango wa “TAKUKURU Rafiki” unaolenga kuwashirikisha wadau mbalimbali katika jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, sambamba na kutekeleza Mkakati wa Habari, Elimu na Mawasiliano (IECS) ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za rushwa na umuhimu wa kuikataa.
Kupitia mkakati huo wa mawasiliano, makundi mbalimbali ya jamii yatafikiwa kwa njia tofauti za uelimishaji na mawasiliano ili kuwahamasisha kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na rushwa.
Vilevile, TAKUKURU imepanga kufanya tafiti na uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma katika sekta muhimu kama ajira, elimu, afya na ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kwa lengo la kubaini maeneo yenye mianya ya rushwa na kupendekeza hatua za kuziba mianya hiyo.
Kwa ujumla, mipango hii inaashiria dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwajibikaji, kuongeza uwazi katika utendaji wa taasisi za umma na kuhakikisha rushwa inadhibitiwa kwa ufanisi ili kuchochea maendeleo ya taifa.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment