Na Mwandishi Wetu, Kahama
SERIKALI ya Kijiji cha Nyanhembe, kilichopo Kata ya Kilago katika Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, imeiomba Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Kahama kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa mifuko ya mawe inayozalishwa katika mgodi mpya ulioibuka hivi karibuni inatolewa ili kuepusha wizi na utoroshaji wa mawe hayo.
Ombi hilo limekuja baada ya kuibuka kwa mgodi wa dhahabu katika eneo hilo, ambapo wananchi wanahofia kuibiwa mawe yao na hivyo kutokufaidika na shughuli za uchimbaji.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Richard Lyatala, ameliambia jopo la waandishi wa habari waliofika katika mgodi huo ili kujionea hali halisi ya mfumuko wa madini kwamba, mgodi huo umeibuka baada ya leseni ya utafiti ya kampuni ya Mwamba Company Limited kuonekana katika kijiji hicho.
Alisema kuwa, mnamo Machi 21, 2026, wananchi walivamia eneo hilo na kuanza shughuli za uchimbaji bila ya kumtambua mwekezaji huyo.
Lyatala aliongeza kuwa, mwekezaji wa kampuni hiyo hakuwasiliana na Serikali ya Kijiji wala kutoa taarifa rasmi kuhusu shughuli za uchimbaji. Hali hii ilisababisha kutokea kwa machafuko ambapo wananchi walikosa ufahamu kuhusu ni nani anawajibika na shughuli hizo.
Vilevile, alisisitiza kuwa, licha ya mgodi kuendelea na uzalishaji wa mawe, mpaka sasa mifuko ya mawe haijauzwa wala kugawanywa, hali inayotishia kuwepo kwa wizi mkubwa na utoroshaji wa mawe ya dhahabu, kwa kuwa wananchi wanaolinda mawe hayo wanategemea ulinzi wa jadi tu, na hakuna malipo rasmi kwa wale wanaolinda.
"Serikali inatakiwa kuchukua hatua ili kuhakikisha wananchi hawawezi kuibiwa mawe yao. Watu wamewekeza fedha zao katika uchimbaji huu na wanahitaji kulipwa kwa haki," alisema Lyatala.
Hata hivyo, Katibu wa Sungudungu wa Kijiji cha Nyanhembe, Lucas Mayunga, alieleza kuwa, mgodi huo umejaa kundi kubwa la watu wanaojiita "manyani", na wanakabiliana na changamoto kubwa ya kuhakikisha mawe ya dhahabu hayatoki kwenye eneo hilo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa, wananchi wanapata hasira kubwa kutokana na kukosa malipo kwa muda wa wiki mbili, huku ulinzi wa jadi ukiwa unakabiliwa na changamoto nyingi.
Mayunga aliiomba Serikali ichukue hatua za haraka ili kuzuia machafuko zaidi.
Pia, alisisitiza kuwa, ni muhimu kuruhusiwa kikundi cha wachimbaji wenye uzoefu na masuala ya madini, ili kiweze kusimamia shughuli za uchimbaji na kuhakikisha serikali inapata maduhuri.
Aliongeza kuwa, mzozo ulipo kati ya wawekezaji na wananchi unahitaji kutatuliwa haraka ili wananchi wa Nyanhembe waweze kunufaika na neema hii ya madini.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Nyanhembe wamepokea kwa ukali kitendo cha mwekezaji Mwamba Company Limited kutofahamika wala kutambulika rasmi kama mmiliki wa leseni ya uchimbaji, hali inayosababisha wasiwasi miongoni mwao.
Wamekemea kitendo cha mwekezaji kuibuka tu baada ya wananchi kuanza kuchimba, na kusema kuwa, licha ya uchimbaji wa mawe kuwa umeanza, bado hawana maelezo ya wazi kuhusu hatima ya mawe yao.
Wananchi hao pia wameomba msaada kutoka kwa Serikali, ili waweze kufaidika na shughuli za uchimbaji na kulipwa haki zao kwa wakati, kabla ya hali hiyo kuendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya kijiji hicho.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa usimamizi wa sheria katika shughuli za uchimbaji wa madini, ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao na kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na utoroshaji wa mawe na wizi wa dhahabu katika mgodi huo mpya.


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment